Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI, THAMINI UHAI WAWEKA MIKAKATI UTEKELEZAJI WA AFUA ZA AFYA YA MAMA NA MTOTO.

Posted on: January 30th, 2026

Na WAF, Dodoma


Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Thamini Uhai, wamekutana kujadili utekelezaji wa mradi wa ushirikiano wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.


Hayo yameelezwa leo Januari 28, 2026 na Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dkt. Ahmad Makuwani, katika uzinduzi wa mradi wa Mama Mjamzito na mtoto salama jijini Dodoma.


Dkt. Makuwani amesema Serikali imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kupunguza vifo vya uzazi kwa kushirikisha wadau mbalimbali ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi.


Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutoa mafunzo kwa wasimamizi na wadau watakaoshiriki katika mradi huo ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miradi kutoka Shirika la Thamini Uhai na Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Dkt. Sunday Dominico, amesema mradi huo wa miaka mitano utatekelezwa katika mikoa ya Kigoma, Katavi na Geita.


Amesema mradi unalenga kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, ikiwemo huduma za dharura za uzazi, huduma kwa watoto njiti na wenye uzito mdogo.


Dkt. Sunday ameongeza kuwa mradi huo unafadhiliwa na Bloomberg Philanthropies na Gates Foundation, wadau wa maendeleo wanaoshirikiana na Serikali katika sekta ya afya.


Amesema wadau hao wataweka mfumo wa pamoja wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa mradi ili kuhakikisha malengo ya kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua yanafikiwa.


Kwa upande Mkurugenzi wa shirika la thamini uhai amesema Tunaenda kutekeleza mradi ambao tutahakikisha huduma za mama na mtoto unaimarishwa.