Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI KUJA NA MWONGOZO WA KUIMARISHA USHIRIKISHWAJI JAMII KATIKA MASUALA YA AFYA

Posted on: October 22nd, 2025

Na.WAF, Dar es Salaam.

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais- TAMISEMI pamoja na wadau mbalimbali iko mbioni kukamilisha Mwongozo wa Kitaifa wa Uhamasishaji Jamii (National Community
Engagement Guideline).

Akizungumza katika kikao kazi cha kupitia Mwongozo huo Oktoba 20, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ona Machangu amesema lengo la kikao hicho ni kuhakikisha kunakuwa na mwongozo wa kitaifa utakaorahisisha ushirikishwaji wa Makundi mbalimbali katika jamii ili kuimarisha uwajibikaji, uwazi na ushiriki wa jamii katika kukinga, kulinda na kuboresha afya zao.

"Kupitia Mwongozo huu tunaendelea kujenga jamii yenye afya bora, inayoshiriki kikamilifu katika maendeleo ya endelevu katika huduma za afya, lishe na ustawi wa jamii ili kufikia Dira ya Taifa 2050," amesema Dkt. Machangu.

Aidha, Dkt. Machangu amesema Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wamekuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Afya ikiwemo Mpango wa Taifa wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, Malaria, Mpango wa Kudhibiti UKIMWI na Mpango wa Taifa wa Magonjwa Yaliyokuwa hayapewi Kipaumbele.

Kikao hicho kimeratibiwa na Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu pamoja na wadau wakiwemo Shirika la Afya DUNIANI( WHO), Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani(UNICEF), Amref Tanzania, Action Against Hunger, SIKIKA na Tanzania Red Cross Society.