MADAKTARI BINGWA WATAKIWA KUTOA ELIMU KUJIKINGA NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA
Posted on: October 20th, 2025
Na. WAF, Mwanza
Madaktari bingwa wa Rais Samia wametakiwa kuweka nguvu katika kutoa elimu kwa wananchi wanaofika kupata huduma mbalimbali namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ikiwa ni pamoja na kuzingatia mlo unaofaa na kujiepusha na tabia hatarishi.
Hayo yameesemwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana Oktoba 20,2025, jijini Mwanza wakati akiwakaribisha Madaktari bingwa wa Rais Samia 58 watakaotoa huduma katika Hospitali za wilaya zote za Mkoa huo kwa siku sita.
Bw. Elikana, ameeleza kuwa Mkoa wa Mwanza unasumbuliwa na magonjwa yasiyoambukiza hivyo amewaomba Madaktari bingwa hao wanapokutana na wagonjwa watumie fursa hiyo kutoa elimu ya namna ya kujiepusha na magonjwa hayo na kuishi kwa kufuata mfumo bora wa maisha kwa kuzingatia milo iliyo sahihi na kuacha tabia bwete.
Aidha, Bw. Elikana amewataka madaktari bingwa wa Rais Samia kutumia ujuzi walionao katika kuwafundisha wataalam walio katika vituo jinsi ya kuhudumia mama mjamzito pamoja na mtoto mchanga ili kuhakikisha vifo vya mama na mtoto vinaendelea kupungua.
“Vifo vya mama na mtoto vimepungua kutoa vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi kufika vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022, hivyo basi uwepo wenu mwaza tunatumaini tutanufaika kwa kutupa ujuzi na mbinu za kuzidi kupunguza na tufike sifuri kabisa jambo ambalo litainua mkoa na Taifa kiujumla,” amesema Bw. Elikana
Kwa upande wake Afisa wa Wizara ya Afya kutoka Idara ya huduma za afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Bi. Fidia Obimbo amesema kambi za madaktari bingwa zimekuwa zikileta tija kubwa kwa wananchi kwa kuwapatia huduma karibu na maeneo yao lakini pia kufanya mafunzo kwa wataalam wengine walioko vituoni hali iliyochangia kuzidi kuboresha huduma za afya.
“Tumekuwa tukifanya uchunguzi na kujua ni kada ipi inahitajika zaidi mfano, awali wataalam wa kinywa na meno, wauguzi na ukunga na usingizi na nganzi salama walikuwa hawapo kwenye seti lakini baada ya kuona uhitaji wao tumewaweka na wamekuwa wakifanya vizuri. Lengo lingine ni wataalam kufundishwa namna ya kutumia vifaa vilivyopo vituo vya afya ili viweze kuwatatulia matatizo ya kiafya wananchi,” amesema Bi. Fidea