Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA KUTOA HUDUMA ZA KIBINGWA NA BOBEZI KAGERA

Posted on: October 21st, 2025

NA WAF – KAGERA

Jumla ya madaktari bingwa na ubingwa bobezi 48 wamewasili mkoani Kagera kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi katika wilaya nane (8) za mkoa huo.

Akizungumza leo Oktoba 20, 2025, mara baada ya kuwapokea madaktari hao, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dkt. Samwel Laizer, amesema ujio wa madaktari hao ni sehemu ya jitihada za Serikali za kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi, hususan wale wa maeneo ya pembezoni.

Dkt. Laizer amesema kuwa katika kambi zilizopita, zaidi ya wananchi 6,000 walipatiwa huduma za kibingwa, na kuongeza kuwa awamu hii inalenga kuwafikia wananchi wengi zaidi.

“Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizi bila kulazimika kusafiri umbali mrefu, jambo linalopunguza gharama na muda. Tunawaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma katika hospitali za wilaya zilizo karibu nao,” amesema Dkt. Laizer.

Kwa upande wake, Dkt. Patrick Kushoka, mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, amesema madaktari hao wanatoka katika fani mbalimbali ikiwemo upasuaji, meno na kinywa, afya ya uzazi, magonjwa ya watoto, magonjwa ya ndani, magonjwa ya njia ya mkojo, pamoja na usingizi na ganzi salama.

“Tutahakikisha huduma hizi za kibingwa zinawafikia wananchi wote katika halmashauri za mkoa wa Kagera. Tunawaalika wananchi kujitokeza katika hospitali zetu za wilaya ili wapate huduma hizi,” amesema Dkt. Kushoka.

Ameongeza kuwa huduma za upasuaji mbalimbali zitafanyika katika hospitali za wilaya kulingana na mahitaji yatakayojitokeza.

Aidha, Dkt. Kushoka amesema kuwa mbali na kutoa huduma, kambi hiyo inalenga pia kujengea uwezo madaktari na wauguzi wa hospitali husika ili waweze kuendeleza utoaji wa huduma hizo hata baada ya kambi kumalizika.

Kambi ya _Dkt. Samia Mentorship_ ni awamu ya nne, na imekuwa ikitekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za kibingwa na kuimarisha mfumo wa rufaa nchini, ambapo huduma hizo zinatarajiwa kutolewa kwa kipindi cha siku sita(6) kuanzia Oktoba 20 hadi 25, 2025.