Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WATUMISIHI WA AFYA WAASWA KUTOA USHIRIKIANO KWENYE MAZOEZI YA USIMAMIZI SHIRIKISHI

Posted on: May 26th, 2025

Na WAF - Lindi


Wito umetolewa kwa watumishi wa afya katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini, kutoa ushirikiano kwa timu ya wataalam wanaofanya usimamizi shirikishi wa ukaguzi wa ubora wa huduma za afya ili zoezi hilo liwe la ufanisi hivyo kuendelea kuboresha huduma za afya nchini.


Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya Dkt. Baraka Nzobo, Mei 27, 2025 akiwa wakati wa kikao kazi cha kujipanga na ukaguzi huo ambao unalenga kutatua changamoto zilizopo na kusaidia katika uboreshaji huduma za Afya.


"Ukaguzi huu shirikishi unaangalia maeneo yote ya Hospitali ikiwemo eneo la Rasiliamali watu, ubora wa huduma zinazotolewa, vifaa tiba lakini pia namna gani huduma zinavyotolewa kwa kuzingatia ubora na ili kama kuna changamoto ziweze kutatuliwa," amesema Dkt. Nzobo


Amesema, ukaguzi huo tayari umefanyika katika kituo cha Afya Town Centre, Kituo cha Afya Mnazi mmoja na Banduka Manispaa ya Lindi, lakini pia zoezi hilo linaendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi.


Kwa upande wa Idara ya Utumishi Dkt. Nzobo amebainisha kuwa ukaguzi huo unaangalia kero za watumishi na baadae kuja na majibu ya kero zao lakini pia changamoto zaidi zitapojitokeza zitawasilishwa Ofisi  ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Afya ili ziweze kufanyiwa kazi.


Amesema kuwa ukaguzi huo tofauti na ukaguzi mwingine ni zoezi la pamoja linalolenga kushirikiana kwa pamoja kati ya Wizara na watendaji hospitalini kutatua changamoto zilizopo ili kutoa huduma bora za Afya karibu na wananchi ili kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya sita.