Customer Feedback Centre

Ministry of Health

RAIS SAMIA AENDELEZA UWEKEZAJI AFYA KUPUNGUZA VIFO VYA UZAZI IFIKAPO 2030

Posted on: March 1st, 2026

Na Aisha Swahibu, WAF - Mwanza

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kikamilifu kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ili kufikia malengo endelevu ya Millennia ambapo hadi Mwaka 2030 vifo vitokanavyo na uzazi vinapaswa kufikia 70 kwa Kila vizazi hai 100,000,

Dkt. Samizi ameyasema hayo leo, Februari 28, 2026, wakati wa uzinduzi wa Wodi ya Watoto Wachanga Wagonjwa na Waliozaliwa Kabla ya Wakati (NCU) iliyojengwa kwa kufuata miongozo ya Wizara ya Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba.

Amesema ili kufanikisha dhamira hiyo, Serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto kwa kujenga na kuboresha vituo vyenye uwezo wa kutoa huduma za dharura za upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni (CEmONC), ambapo hadi sasa vituo 580 nchini vina uwezo wa kutoa huduma hizo.

“Serikali imejipanga kuhakikisha vifo vitokanavyo na uzazi vinaendelea kupungua. Sio kuwa na majengo ya hospitali pekee, ndiyo maana Mhe. Rais ameendelea kuajiri watumishi wa afya, kuboresha miundombinu ya barabara ili mama mjamzito afike hospitalini kwa urahisi, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba na wodi za kisasa,” amesema Dkt. Samizi.

Kwa upande wa watoto wachanga Serikali imejipanga kupunguza vifo vya watoto hao kufikia 12 kwa kila vizazi hai 1000, vifo vya watoto umri chini ya miaka mitano kufikia 25 kati ya vizazi hai 1000 hadi kufikia 2030

Ameeleza kuwa jengo la NCU lililozinduliwa ni la kisasa na limezingatia viwango vyote vya Wizara ya Afya, likiwawezesha akina mama kukaa na watoto wao wakati wanapatiwa matibabu, pamoja na kuwapa nafasi baba kushiriki katika malezi na uangalizi wa awali wa mtoto jambo ambalo hapo awali halikuwepo.

Aidha, Dkt. Samizi amesema wodi hiyo itapunguza gharama za matibabu kwa wagonjwa na kupunguza rufaa zisizo za lazima, kwani huduma nyingi zitapatikana moja kwa moja katika hospitali hiyo. Ameongeza kuwa hospitali hiyo itakuwa kituo cha rufaa kwa halmashauri za wilaya zinazopakana na Kwimba.