WATAALAM WA MAABARA WANOLEWA KWA UTAYARI MAGONJWA YA MLIPUKO-EBOLA
Posted on: July 29th, 2026Na Zakayo Mosha WAF-Katavi
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI pamoja na Shirika la Afya duniani (WHO) imeendelea kutoa mafunzo ya utayari kwa Wataalam wa Maabara kwa Mikoa ya Katavi, Songwe, Kigoma na Rukwa shabaha ikiwa kukabiliana na hatari ya kuzuka kwa Magonjwa ya mlipuko nchini ikiwemo ugonjwa wa Ebola.
Akifungua mafunzo ya Wataalam wa Maabara kutoka Mikoa hiyo leo Juni 29,2026 mkoani Katavi, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dkt. Jonathan Budenu amewataka Wataalam wa Maabara kutumia mafunzo, ujuzi na mbinu watakazopatiwa kuhakikisha Watanzania wanaendelea kuwa salama.
"Ugonjwa wa EBOLA umeendelea kuwa tishio kwa nchi jirani za DRC na Uganda,hivyo Mikoa ya mipakani kama huu wa Katavi na Mingine Nchini ni lazima tuchukue tahadhari ya kutosha kwa Wataalam wa Afya kuendelea kuwaelimisha Wananchi na wenyewe kuchukua tahadhari za kujikinga" amesema Dkt. Jonathan.
Dkt. Jonathan amewasisitiza Wataalam wa Maabara waliopata nafasi ya kupata mafunzo hayo kwa muda wa siku tano wasiwe wachoyo na wabinafsi bali, washirikiane na wenzao mahali pakazi kuhusu ujuzi na maarifa mapya watakayopata ya namna bora ya kukusanya,kuchambua na kusafirisha sampuli za Magonjwa hatarishi.
"Ili Tanzania Iendelee kuwa salama na magonjwa haya ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu, Maburg, MPOX na Ebola ni wajibu wa Wataalam wa Maabara kuendelea kushirikiana na Wataalam wengine wa Sekta ya Afya pamoja na jamii kwa ujumla kwani jambo hili, bila ushirikiano wa dhati haliwezi kufanikiwa" amesema na kuongeza Dkt. Jonathan
Dkt. Jonathan ameishukuru Wizara ya Afya kwa jinsi ilivyo mbel dhidi ya mapambano ya magonjwa ya mlipuko kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo kama Shirika la Afya duniani (WHO) Pandemic Fund.
"Mkoa wa Katavi tunawashukuru Sana WHO kufanyia mafunzo haya hapa Katavi, tunachukua mafunzo haya kama chachu kwa Wataalam wetu wa Maabara kuimarika zaidi katika ufanisi wa kazi hususani wakati huu ambapo Taifa linachukua tahadhari mbalimbali za kuzuia ugonjwa wa Ebola usiingie Nchini" amesema Dkt.Jonathan.