Ministry of Health

SERIKALI KUENDELEA KUWEKEZA KATIKA MAFUNZO NA AJIRA ZA WATAALAMU WA DAWA ZA USINGIZI NA GANZI

Posted on: June 28th, 2026

Na Shaban Juma, Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika mafunzo, ajira na uboreshaji wa mazingira ya kufundishia wataalamu wa dawa za usingizi na ganzi (Anaesthesia) ili kuhakikisha nchi inakuwa na wataalamu wa kutosha wenye uwezo wa kutoa huduma salama za upasuaji, wagonjwa mahututi na huduma za dharura.

Dkt. Samizi ameyasema hayo leo Juni 27, 2026 wakati akifungua Kongamano la Kisayansi la Tanzania Association of Anaesthesia Students (TAAS) lililofanyika katika Ukumbi wa Taasisi ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), ambapo limewakutanisha wanafunzi, wahadhiri, wataalamu na wadau wa taaluma ya Anaesthesia kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Dkt. Samizi amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wataalamu wa dawa za usingizi na ganzi katika kuhakikisha huduma za upasuaji zinakuwa salama na zenye ubora, hivyo itaendelea kushirikiana na vyuo vikuu, hospitali za kufundishia na wadau mbalimbali kuimarisha mafunzo na mazingira ya kujifunzia.

Amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya vyuo vya afya na hospitali za kufundishia kwa kuongeza vifaa vya kisasa vya kufundishia ikiwemo mashine za Anaesthesia, ventilators, multiparameter monitors, vifaa vya mafunzo ya ICU pamoja na maabara za mafunzo ili kuongeza ubora wa elimu kwa wanafunzi.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuhamasisha wataalamu kuongeza sifa kupitia masomo ya Shahada ya Uzamili na Ubingwa ili kuongeza idadi ya wakufunzi na wataalamu bingwa, huku ikiendelea kushirikiana na Wizara yenye dhamana ya elimu na vyuo vikuu kupanua programu za Shahada, Uzamili na Ubingwa katika taaluma ya Anaesthesia na maeneo yanayohusiana nayo.

Dkt. Samizi amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwekeza katika kuimarisha miundombinu ya hospitali, upatikanaji wa vifaa tiba na dawa muhimu pamoja na rasilimali watu, hatua zinazochangia kuboresha huduma za upasuaji na huduma nyingine za kibingwa nchin