SERIKALI, WADAU KUFANYA TATHMINI YA UBORESHAJI WA UHIFADHI WA CHANJO NA MIFUMO YAKE
Posted on: July 29th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF - Morogoro
Serikali kupitia Wizara ya Afya, OWM - TAMISEMI kwa kushirikiana na 'inSupply Health Tanzania' imeanza tathmini ya utekelezaji wa mradi wa kuboresha mfumo wa uhifadhi wa chanjo na matengenezo ya majokofu ikiwa ni hatua ya kupima mafanikio yaliyopatikana na kuweka mikakati ya kuhakikisha matokeo ya mradi yanaendelea kuwa endelevu baada ya kumalizika kwa mradi huo.
Dkt. Florian Tinuga kutoka Idara ya Huduma za Afya, Kitengo cha Huduma za Kinga, OWM - TAMISEMI amesema hayo leo Juni 29, 2026 wakati akimwakilisha Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo Dkt. Georgina Joachim kutoka Wizara ya Afya wakati akifungua kikao kazi cha tathmini ya utekelezaji wa mradi huo kilichofanyika mkoani Morogoro.
"Tumekusanyika leo kwa lengo kubwa la kufanya tathmini inayolenga kujadili kwa pamoja mafanikio, changamoto na hatua zitakazochukuliwa ili kuendeleza maboresho yaliyopatikana katika mradi wa 'Rapid Repair and Response (R3)' usajiri na usimamizi wa matengenezo ya majokofu ya chanjo na vifaa vya mnyororo baridi nchini baada ya kumalizika mda wake," amesema Dkt. Tinuga
Amesema, mafanikio yaliyopatikana katika mradi huo ni pamoja na kujenga uwezo wa watumishi wa afya katika ngazi za vituo vya kutolea huduma, Timu za Usimamizi wa Afya za Halmashauri (CHMT) na Timu za Usimamizi wa Afya za Mikoa (RHMT), ili kuimarisha usimamizi, utunzaji na matengenezo ya majokofu yanayotumika kuhifadhi chanjo.
Aidha, Dkt. Tinuga amesema kuwa moja ya changamoto zilizokuwepo kabla ya utekelezaji wa mradi ilikuwa ni kutokuwepo kwa mfumo madhubuti wa kurekodi matengenezo ya majokofu, hali iliyokuwa ikisababisha ugumu katika kufuatilia historia ya hitilafu na hatua zilizochukuliwa ili kuweza kuzitatua.
"Kikao hiki pia tunatarajia kitatoa nafasi kwa washiriki kutoka mikoa, halmashauri na vituo vya kutolea huduma kushirikishana uzoefu na kutoa mapendekezo yatakayosaidia Serikali kuimarisha zaidi mfumo wa usimamizi wa vifaa vya mnyororo baridi na uhifadhi wa chanjo nchini," amesema Dkt. Tinuga