Customer Feedback Centre

Ministry of Health

ZANZIBAR, TANZANIA BARA WAUNGANISHA NGUVU KUBORESHA MAWASILIANO YA SERIKALI, ELIMU YA AFYA KWA UMMA

Posted on: February 26th, 2026

Na Atley Kuni, WAF- Dodoma

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeendeleza ushirikiano wao katika sekta ya afya kupitia ziara ya kikazi iliyolenga kuboresha mawasiliano ya umma na elimu ya afya kwa jamii.

Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya Zanzibar imefanya ziara ya siku tano katika Wizara ya Afya Tanzania Bara, jijini Dodoma, kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha utendaji kazi wa nyanja za mawasiliano ya serikali na uhamasishaji wa afya kwa umma.

Ziara hiyo iliyoanzia Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (GCU) kilichopo Mji wa Serikali Mtumba, ambapo ujumbe huo ulipata maelezo ya kina kuhusu muundo wa kitengo, mfumo wa uratibu wa mawasiliano, usimamizi wa ratiba za viongozi, pamoja na namna taarifa za afya zinavyoratibiwa na kufikishwa kwa wananchi kwa wakati na kwa ufanisi.

Katika hatua nyingine, ujumbe huo ulikutana na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Dkt. Amour Selemani, katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Mazungumzo yao yalijikita katika kuimarisha mikakati ya huduma za kinga, kuendeleza afua za mabadiliko ya tabia kwa jamii, na kuongeza matumizi ya mawasiliano ya kimkakati ili kufanikisha kampeni za afya.

Pande zote mbili zilikubaliana kuandaa Mpango wa Ushirikiano (Collaboration Plan) utakaoainisha maeneo ya kipaumbele, mgawanyo wa majukumu, mfumo wa utekelezaji na ratiba ya shughuli za pamoja.

Katika hatua nyingine ilikubaliwa kuwa Wizara ya Afya Tanzania Bara itafanya ziara ya kikazi Zanzibar katika kipindi kijacho ili kuendeleza mchakato wa kujifunza na kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Uhamasishaji (HPU) kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Gora Faki Haji, alisema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa kuwapatia fursa ya kujifunza mbinu bora za uhamasishaji, usimamizi wa mawasiliano ya kimkakati na utoaji wa elimu ya afya kwa umma kwa njia shirikishi na za kisasa.

Kwa upande wake Afisa Uhusiano, Bi. Sabia Abeid Hemed, amesema kuwa uzoefu walioupata utaongeza ufanisi wa uratibu wa taarifa na kuimarisha mawasilia