Customer Feedback Centre

Ministry of Health

ELIMU YA LISHE ITOLEWE NA WANATAALUMA WA LISHE KUEPUKA UPOTOSHAJI

Posted on: February 27th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF - Dodoma

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amewataka wanataaluma wa lishe nchini kutoa elimu sahihi kwa wananchi kwa viwango vinavyokubalika ili jamii ione faida ya uwepo wa wanataaluma hao.

Dkt. Magembe amesema hayo leo Februari 26, 2026 alipokua anafungua Mkutano Mkuu wa Nne wa Chama cha Wataalamu wa Lishe Tanzania 2026 uliofanyika katika ukumbi wa Mabeyo Mkoani Dodoma.

"Sasa hivi, huko kwenye mitandao ya kijamii kuna watu ambao si wataalamu wa lishe lakini wanatoa elimu ya lishe ambayo si sahihi, nyinyi ndio wataalamu msiache wananchi wapewe taarifa potofu kwa sabau madhara yake kiafya ni makubwa," amesema Dkt. Magembe

Amesema, jamii inatakiwa kupata elimu sahihi, ujumbe sahihi, kujua nini na kwa wakati gani chakula kipi kinafaa kuliwa, vitu gani visiliwe na kwa wakati gani, hii itapelekea kupata taifa lenye afya bora.

Aidha, Dkt. Magembe amewataka wanataaluma hao kufanya tafiti ili kujua chanzo cha matatizo ya lishe nchini katika Mikoa mbalimbali kwa sababu matatizo ya lishe yanayofautiana kati ya jamii moja na nyingine.

"Hakuna taaluma yoyote katika Sekta ya Afya ambayo inaweza kutoa majibu ya changamoto za wananchi bila kufanya tafiti, amesema Dkt. Magembe
Aidha, amewakumbusha wataalamu kutumia fursa za wagonjwa na ndugu zao wanapokuja kutibiwa katika hospitali, kuwapa elimu ya kishe bora and na namna ya kutumia chakula kama sehemu ya tiba.