WANANCHI WA SONGWE WACHANGAMKIA FURSA YA MATIBABU YA UPASUAJI WA MTOTO WA JICHO
Posted on: February 25th, 2026Na Cletus Sanga, WAF – Songwe
Kambi maalumu ya upasuaji wa mtoto wa jicho inaendelea mkoani Songwe ikiwa ni siku ya nne (4), ambapo zaidi ya Wagonjwa 350 tayari yamefanyiwa upasuaji. Lengo la kambi hiyo ni kufikia wagonjwa 500 ndani ya siku sita (6), ili kutatua changamoto ya uoni kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na ugonjwa wa mtoto wa jicho, ambao unatibika.
Hayo yameelezwa leo tarehe 24 Februari, 2026 na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Boniface Kasululu, wakati kambi hiyo ikiendelea katika Hospitali ya Wilaya ya Vwawa, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe.
“Ili kuwafikia wahitaji, tumetumia mbinu ya kuwafuatilia kaya kwa kaya kwa msaada wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii. Njia hii imewezesha kuwabaini wananchi wengi waliokuwa wakihitaji matibabu lakini hawakuwa na taarifa sahihi. Ushirikiano wa karibu na jamii umeongeza ufanisi wa zoezi hili,” ameongeza
Dkt. Kasululu amewahimiza wakazi wa Songwe kujitokeza kwa wingi kutumia huduma hizo tembezi, akisisitiza kuwa zinapatikana bila gharama yoyote.
Kwa upande wake, Afisa Mradi wa Shirika la Kimataifa la Helen Keller, Bw. Allen Lemilia, amesema amesema huduma hiyo inawafikia wakazi wote wa mkoa wa Songwe, huku usafiri ukiandaliwa kwa ajili ya kuwachukua walengwa na kuwaleta hospitalini baada ya kutambuliwa na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka TAMISEMI, Dkt. Kalidushi Kubingwa, amesema Serikali imeboresha miundombinu katika hospitali za wilaya, ikiwemo vyumba vya upasuaji (theatre), hatua inayorahisisha utoaji wa huduma za upasuaji katika ngazi ya wilaya.
Aidha, Dkt. Kubingwa ameushukuru uongozi wa Wilaya ya Mbozi kwa ushirikiano wanaoutoa katika kampeni hiyo, na pia kuishukuru taasisi ya Helen Keller International kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kusogeza karibu huduma za matibabu ya upasuaji wa mtoto wa jicho zinazotolewa bila malipo.