WATAALAM WA AFYA, MAZINGIRA WAPIGWA MSASA ARUSHA
Posted on: August 14th, 2025
Na WAF – ARUSHA
Maafisa Afya na Usafi wa Mazingira wa mkoa na Jiji la Arusha wamepewa mafunzo ya kulinda afya, usalama na utu wa wafanyakazi wa utoaji wa huduma za usafi wa mazingira nchini ambayo yana lengo la kuwaongezea ujuzi na weledi katika kutekeleza majukumu yao.
Akifungua mafunzo hayo Agosti 13, 2025, Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Change Ntulwe, amesema mafunzo hayo yatasaidia kuongeza weledi kwa maafisa afya ambao wana jukumu la kusimamia usafi wa mazingira jijini Arusha.
“Suala la afya, usalama na utu, wa watoa huduma za usafi wa mazingira wanapotoa huduma hizo katika jamii ni jambo linalopaswa kutiliwa umuhimu sana, kwani wao pia ni sehemu ya jamii na pia ni muhimu kuzingatia kanuni za afya na usalama kwa lengo la kuzuia kusambaa kwa magonjwa katika jamii,” amesema Dkt. Ntulwe.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo maafisa afya katika sehemu kuu tatu za afya, usalama na utu ili kuhakikisha kuwa wafanyakazi hawa wanalindwa wakati wa utekelezaji wa majukumu.
Naye, Mratibu wa Kitaifa wa Usalama na Afya mahala pa kazi kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO) Bi. Getrude Sima amesema shirika hilo linatambua umuhimu wa maafisa afya na mazingira pamoja na wafanyakazi wanaohusika kusafisha mazingira kutokana na aina ya huduma wanazozitoa.
Ameongeza kuwa mara nyingi wafanyakazi hawa huwa wanashindwa kudai stahiki zao wanapoumia kazini au baada ya kutoa huduma hizo kutokana na kuwa ni sekta isiyo rasmi na kukosekana kwa usimamizi na utetezi katika kusimamia maslahi yao.