Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WATAALAM USAFI WA MAZINGIRA WAPONGEZWA KWA KAZI KUBWA YA KUTUNZA MAZINGIRA

Posted on: August 15th, 2025

Na WAF – Arusha

Wataalam wa usafi wa mazingira mkoani Arusha wamepongezwa kutokana na uthubutu wa kufanya kazi ya kutunza mazingira na kufanya miji kuwa safi muda wote.

Pongezi hizo zimetolewa Agosti 14, 2025, na Mganga Mkuu wa mkoa wa Arusha Dkt. Charles Mkombachepa wakati akizungumza na wafanyakazi wa usafi wa mazingira mkoani Arusha ambao wanapewa mafunzo ya afya, usalama na utu kwa wafanyakazi wa usafi wa mazingira.

Dkt. Mkombachepa amesema suala la afya, usalama na utu wa watoa huduma za usafi wa mazingira wanapokuwa wakitoa huduma hizo ndani ya jamii, ni jambo linalopaswa kutiliwa mkazo kwani wao pia ni sehemu ya jamii na pia ni muhimu kuzingatia kanuni za afya na usalama kwa lengo la kuzuia kusambaa kwa magonjwa katika jamii.

“Wafanyakazi wa usafi au kwa kiswahili sanifu Matopasi, ni jamii ya wafanyakazi ambao wanakutana na changamoto nyingi wakati wakiwa wanatoa huduma hii muhimu katika jamii yetu. Miongoni mwa changamoto wanazokumbana nazo ni pamoja na unyanyapaa, mazingira duni ya kazi, ujira kidogo na vifaa duni vya kazi,” amesema Dkt. Mkombachepa.

Ameongeza kuwa mara nyingi wafanyakazi hao huwa wanashindwa kudai stahiki zao baada ya kutoa huduma hizi kutokana na kuwa ni sekta isiyo rasmi na kukosekana kwa usimamizi na utetezi katika kusimamia maslahi yao.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Afya kwa ushirikiano na Shirika la Kazi Duniani (ILO), Benki ya Dunia, SNV na Water Aid Tanzania.