Ministry of Health

WADAU KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI MAPAMBANO DHIDI YA UGONJWA WA SIKOSELI NCHINI

Posted on: August 18th, 2026

Na Zakayo Mosha, WAF-Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya imewaomba wadau wa ndani na nje ya nchi kujitokeza katika mapambano ya kutokomeza ugonjwa wa Sikoseli nchini hadi kufikia 2050, kwa lengo la kujenga jamii imara na yenye afya bora kwa maendeleo ya familia na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa leo Agosti 19, 2026 Jijini Dodoma na Dkt. Eliud Eliakimu Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali wakati akifunga kikao kazi cha wadau mbalimbali wanaohusika na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Sikoseli hapa nchini.

Amesema Wizara ya Afya inatambua mchango wa wadau katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Sikoseli, amesisitiza Serikali kuendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali katika kuelimisha jamii ya Watanzania.

"Naomba kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa niwashukuru kwa ushirikiano wenu pamoja na juhudi kubwa mnazofanya kushirikiana na Serikali katika kuelimisha umma hususani vijana kuelewa jinsi ya kuzuia kwa kupima Afya kwa kutambua kama wana vinasaba kabla hawajaamua kuzaa watoto", amesema Dkt. Eliud.

Aidha, amewataka Wataalam wa afya katika ngazi zote za kutolea huduma kuendelea kushirikiana na Wadau katika kuelimisha Wananchi zaidi kuelewa kuhusu chanzo,dalili na njia za kuzuia ugonjwa wa Sikoseli.

Awali akizungumza Dkt. Asteria Mpoto Mratibu wa huduma za Sikoseli Wizara ya Afya, amewaomba wadau wengi zaidi kujitokeza kusaidiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya katika juhudi za kutomeza ugongwa huo katika jamii ya Watanzania. amesisitiza kufanya kazi kwa umoja,mshikamano na upendo ili kufikia mikakati tuliyojiwekea.

Kwa upande mwingine, Dkt.Robhi Jeremiah kutoka Taasisi ya Ruge Mutahana Foundation ambaye pia ni Mwakilishi Mdau upande wa Vijana,amesema Vijana hapa Nchini bado wanahitaji elimu zaidi ya kuelewa kwa kina kuhusu Ugonjwa wa Sikoseli.

Amesema, Vijana ndiyo walengwa wakubwa katika Jambo hili kwani ndiyo wanaotegemea kuoa au kuolewa pamoja na kuzaa watoto,pia ameishukuru Wizara ya Afya kwa jinsi inavyotoa ushirikiano kwa wadau ikiwa ni pamoja na Miongozo muhimu ya Kitaifa ya mapambano dhidi ya Sikoseli.