TUHAMASISHANE KWENDA HOPITALI KWA WENYE DALILI ZA TRAKOMA
Posted on: September 18th, 2024
Na WAF - Dar Es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ametoa rai kwa Watanzania hasa wa Mkoa wa Pwani kushirikiana na Serikali kumhamasisha mwananchi yeyote mwenye dalili za ugonjwa wa Macho kwenda Hospitali kwakuwa ugonjwa huo husababisha upofu.
Waziri Mhagama amesema hayo leo Septemba 18, 2024 wakati wakiwa katika ziara pamoja na Princess Sophie (Duchess of Edinburgh) ambae ni Mke wa Mtoto wa Mfalme wa Uingereza walipotembelea Kituo Cha Afya cha Mlandizi Mkoa wa Pwani kwa lengo la kujionea utoaji huduma za matibabu ya macho
“Yapo magonjwa ambayo hayajapewa kipaumbele sio Tanzania tu bali Duniani kote ikiwemo ugonjwa huu wa macho ( Trakoma) lakini pia magonjwa kama mabusha , matende, minyoo ya tumbo, kichocho.” Amesema Waziri Mhagama
Waziri Mhagama amshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali ya Uingereza kwa kuamua kufanya kazi ya kutokomeza magonjwa haya amabyo hayapewi kipaumbele.
Kwa upande wake, Princess Sophie (Duchess of Edinburgh) ambae ni Mke wa Mtoto wa Mfalme wa Uingereza amesema lengo lao ni kuhakikisha Tanzania inatokomeza magonjwa yasiyopewa Kipaumbele.
“Haya yote yanawezekana kupitia ushirikiano ambao tunautoa kwa Tanzania ikiwa ni kwa mtu mmoja mmoja katika kutokomeza magonjwa ya Trakoma.” Amesema Bi. Sophie
Amesema, Kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Serikali ya Uingereza, kwa pamoja wanaweza kutokomeza ugonjwa huo wa Trakoma kutokana na uzoefu wa magonjwa mengine waliyoweza kuyatokomeza.
Ziara hiyo imemalizika kwa kumtembelea nyumbani kwake mnufaika wa matibabu ya Ugonjwa wa Trakoma yanayotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau akiwemo Sightsavers.