Ministry of Health

SERIKALI YAWEKA MIKAKATI KUONGEZA UZALISHAJI WA DAWA NA VIFAA TIBA NCHINI

Posted on: October 13th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Dodoma

Serikali inaendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza uzalishaji wa dawa na vifaa tiba nchini ili kupunguza utegemezi wa bidhaa hizo kutoka nje na kuimarisha upatikanaji wake kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha sekta ya afya nchini.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu, Dkt. Grace Magembe, leo, Oktoba 13, 2026, jijini Dodoma, wakati akiwasilisha taarifa hiyo katika kamati ya kudumu ya bunge ya afya na masuala ya UKIMWI

Dkt. Magembe amesema uzalishaji wa ndani kwa sasa unakidhi takribani asilimia 20 ya mahitaji ya bidhaa za afya, huku zaidi ya asilimia 80 ya mahitaji hayo yakitegemea bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.

Serikali inalenga kuongeza uzalishaji wa ndani ili kukidhi zaidi ya asilimia 60 ya mahitaji ya taifa ifikapo mwaka 2030. Katika kufikia lengo hilo, Wizara imeanzisha Kikosi Kazi Maalumu cha Kuharakisha Uwekezaji katika Sekta ya Dawa na Vifaa Tiba (PIAT), kinachoratibu wawekezaji na kusaidia kuondoa vikwazo vinavyoweza kuchelewesha utekelezaji wa miradi.

Hatua nyingine ni kuendeleza Kongani Maalumu ya Viwanda vya Dawa na Vifaa Tiba Mloganzila, ambako ekari 386 kati ya 400 zimetolewa kwa wawekezaji 11 waliokidhi vigezo. Aidha, wawekezaji wengine wanaendelea na maandalizi ya kujenga viwanda katika maeneo mbalimbali nchini.

Utekelezaji wa mikakati hiyo unalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa ndani, kuimarisha upatikanaji wa bidhaa muhimu za afya na kujenga mazingira yatakayowezesha Tanzania kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na masoko ya kikanda.

Amesema Serikali pia inaendelea kushughulikia changamoto za miundombinu, upatikanaji wa mitaji, teknolojia na malighafi, pamoja na kuimarisha mifumo ya uwekezaji na masoko kwa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Dkt. Magembe amesema juhudi hizo zinaendana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu umuhimu wa kuimarisha uzalishaji wa dawa na vifaa tiba nchini, na azma ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.