Ministry of Health

KAMATI YA BUNGE YATAKA USHIRIKIANO WA SEKTA MTAMBUKA KUIMARISHA LISHE NCHINI

Posted on: October 15th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imehimiza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na wizara nyingine za kisekta katika kutatua changamoto za lishe nchini, ikisisitiza umuhimu wa kuweka kipaumbele katika changamoto zinazoweza kutatuliwa kwa urahisi ili kuboresha hali ya lishe kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa majadiliano ya taarifa ya Wizara ya Afya kuhusu mpango na mkakati wa kuimarisha lishe nchini leo Oktoba 15 2026, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Zeyana Hamid, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha upatikanaji wa takwimu sahihi na kufanya tafiti zitakazobaini changamoto za lishe nchini pamoja na kupendekeza suluhisho zinazoweza kutekelezwa ili kuhakikisha wananchi wanapata lishe bora.

Aidha, Kamati imesisitiza umuhimu wa kuimarisha Taasisi ya Chakula na Lishe ili iweze kuratibu na kuunganisha sekta zote zinazohusika na masuala ya lishe nchini, zikiwemo sekta za afya, kilimo, usafirishaji, biashara na elimu, kwa lengo la kuhakikisha kila sekta inatekeleza wajibu wake katika kukabiliana na changamoto za lishe.

Vilevile, Kamati imehimiza kukamilishwa kwa Sera ya Chakula na Lishe ili kuweka mwongozo madhubuti wa kisera utakaosaidia kuimarisha uratibu na utekelezaji wa mipango ya lishe nchini, sambamba na kuweka wazi wajibu wa kila sekta katika kufanikisha azma hiyo.

Katika hatua nyingine, Kamati imesisitiza umuhimu wa kuimarisha upatikanaji wa wataalamu wa lishe na kuweka mikakati ya kukabiliana na upungufu wao ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za lishe. Kamati pia imeeleza umuhimu wa kuzingatia uhusiano kati ya lishe na huduma za afya, hususan namna hali ya lishe ya mgonjwa inavyoweza kuzingatiwa katika uchunguzi, matibabu na ushauri wa kitaalamu.

Sambamba na hayo, Kamati imehimiza kuimarishwa kwa urutubishaji wa vyakula kwa kuongeza vitamini na madini muhimu, huku ikisisitiza matumizi ya vyakula vya asili vinavyopatikana katika mazingira ya jamii kama sehemu ya juhudi za kuboresha lishe na afya za wananchi.