KAMATI YA BUNGE YAAHIDI KUUNGA MKONO SERIKALI KUIMARISHA VIWANDA VYA DAWA NA VIFAA TIBA
Posted on: October 13th, 2026Na Shaban Juma, WAF – Dodoma
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Zeyana Hamid, amesema Kamati hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kuimarisha viwanda vya ndani vya dawa na vifaa tiba ili kuongeza uzalishaji nchini na kupunguza utegemezi wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.
Hayo ameyasema oktoba 13,2026 jijini Dodoma na kusisitiza kuwa Kamati iko tayari wakati wowote kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha azma ya kuongeza uzalishaji wa dawa na vifaa tiba nchini inafikiwa, akisisitiza kuwa uwepo wa viwanda imara ni muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa hizo kwa wakati, kuimarisha huduma za afya na kulinda afya za wananchi.
Dkt. Hamid ameeleza kuwa Kamati itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuisimamia Serikali, kutoa ushauri na kuunga mkono mipango na mikakati ya Wizara ya Afya inayolenga kuimarisha uzalishaji wa ndani, huku ikisisitiza umuhimu wa kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji na kuhakikisha viwanda vilivyopo vinaimarishwa na kuongeza uwezo wake wa uzalishaji.
Aidha, kwa niaba ya Kamati, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka kipaumbele katika maendeleo ya sekta ya afya, hususan juhudi za kuimarisha uzalishaji wa dawa na vifaa tiba nchini.
Amesema uwekezaji katika viwanda hivyo una umuhimu mkubwa kwa kuwa utasaidia kupunguza gharama za uagizaji wa bidhaa za afya kutoka nje, kuokoa fedha za kigeni, kuongeza fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi, sambamba na kuhakikisha wananchi wanapata dawa na vifaa tiba vinavyohitajika katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Bw. Emmanuel Daud Tayari, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha mazingira ya uzalishaji wa ndani ili kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba na kuifanya Tanzania kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.