Ministry of Health

SERIKALI YATAKA MAAZIMIO YA KONGAMANO LA VIJANA KUTEKELEZWA KWA VITENDO

Posted on: October 14th, 2026

Na Mvuda Jaffer, WAF-Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya afya imesisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma rafiki za afya ya uzazi, afya ya akili na ulinzi wa vijana dhidi ya ukatili wa kijinsia, huku ikihimiza ushirikiano wa sekta mbalimbali katika kuhakikisha vijana wanapata taarifa sahihi na huduma bora za afya nchini.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 14, 2026, na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya Dkt.Mzee Nassoro akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya alipokuwa akihutubia kabla ya kufunga rasmi Kongamano la Vijana lililolenga kujadili masuala ya afya na ustawi wa vijana.

“Vijana ndiyo nguvu kazi, wabunifu na viongozi wa sasa na wa baadaye wa Taifa letu. Kuwekeza katika afya zao ni uwekezaji wa kimkakati kwa maendeleo endelevu ya rasilimali watu nchini.” amesema Dkt. Nassoro

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha vijana wanapata taarifa sahihi na huduma bora za afya, huku ikitambua changamoto zinazohitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali.

Akizungumzia huduma rafiki za afya ya uzazi, ameeleza umuhimu wa kuhakikisha vijana balehe wanapata huduma bora, salama na zinazolinda siri zao, huku akiwataka watoa huduma za afya kuzingatia weledi na kutobagua vijana.

Aidha, amesisitiza matumizi ya mifumo ya kidijitali, shule, vyuo na mazingira ya jamii katika kuimarisha utoaji wa elimu ya afya inayowafikia vijana kwa urahisi.

“Kuhusu afya ya akili, changamoto za kiuchumi, msongo wa mawazo na unyanyapaa zinaweza kuathiri ustawi wa vijana, hivyo ni muhimu kuimarisha huduma za afya ya akili katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na kuongeza uwezo wa wataalamu. “amesema Dkt.Nassoro

Amewahimiza wazazi, walezi, taasisi za elimu na jamii kushirikiana kutambua changamoto hizo mapema na kujenga mazingira ya kuwasikiliza na kuwasaidia vijana.