SERIKALI INATAMBUA MCHANGO WA SEKTA BINAFSI KATIKA KUWAHUDUMIA WANANCHI
Posted on: February 18th, 2024
Na. WAF - Dar Es Salaam
Serikali kupitia Wizara ya Afya imebainisha kuwa inatambua na kuthamini mchango wa Sekta binafsi katika nyanja zote kupitia utekelezaji sera ya ubia kati ya Sekta za Umma na Binafsi (P-P-P) ambapo imevutiwa na uwekezaji unaofanywa nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo Februari 18, 2024 kwenye uzinduzi wa Hospitali ya Saifee iliyozinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa jijini Dar Es Salaam.
“Sisi Kama Serikali tunashirikiana na Hospitali zote binafsi ikiwemo hii ya Saifee katika kuvutia wagonjwa kutoka nje ya nchi na tunaendelea kuondoa vikwazo vinavyokwaza Sekta binafsi katika kutoa huduma za Afya nchini.” Amesema Waziri Ummy.
Waziri @ummymwalimu amesema, Serikali inaendelea kushirikiana na Sekta Binafsi ikiwemo Hospitali hiyo ya Saifee katika kuvutia wagonjwa kutoka nje ya nchi ambapo hivi sasa zipo Hospitali Sita zinazotoa huduma za Tiba Utalii ikiwemo za Serikali na binafsi.
“HospitalI hizo ni pamoja na Muhimbili, MOI, JKCI, Ocean Road, Saifee na Aga Khan ambapo Hospitali hizo zimeweza kuona na kutibu wagonjwa kutoka nje ya nchi kwa mwaka 2022 walionwa wagonjwa 5,705 na mwaka 2023 wameongezeka na kufikia wagonjwa 6,931 waliopata matibabu sawa na ongezeko la wagonjwa 1,226.” Amesema Waziri Ummy
Mwisho, Waziri Ummy ametoa rai kwa Watanzania kuzingatia mtindo bora wa maisha ikiwemo kufanya mazoezi, kuacha matumizi ya vyakula kwa kuongeza mafuta mengi, chumvi nyingi na sukari kupita kiasi.
“Hata kama tutajenga hospitali 100 kama hizi za Saifee tusipobadili mtindo wetu wa maisha hospitali hazitatosha tusifanye mzaha na ushauri tunaopata kutoka kwa wataalamu wa Afya akiwemo Dkt. Janabi.” Amesema Waziri Ummy