Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI, HOSPITALI ARUSHA LUTHERAN KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: January 24th, 2025

Na WAF, DODOMA

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Mhe. Elibariki Kingu, ameiagiza Wizara ya Afya kuchukua hatua za haraka kuingia makubaliano na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center kwa lengo la kuzisaidia kwa ruzuku, vifaa tiba, dawa, na wahudumu wa afya.

Mhe. Kingu ametoa agizo hilo Januari 23, 2025 wakati wa kikao cha kamati kilichofanyika baada ya wasilisho la Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center, ambayo imeelezea mafanikio yake ya utoaji wa huduma za afya kwa miongo kadhaa, hivyo ni muhimu kushirikiana na Serikali ili kuboresha sekta ya afya.

Kamati hiyo pia imetoa mapendekezo ya kuboresha ufanisi wa huduma hizo, ikiwemo kufunga mifumo ya kielektroniki ya afya (EHMS) kwani hospitali zinapaswa kufungwa mfumo huo ili kudhibiti ubadhirifu wa fedha na kuondoa malipo ya fedha mkononi, akitolea mfano wa mafanikio ya mfumo huo katika Hospitali ya KCMC.

Aidha Mhe. Kingu amesema Kamati imependekeza NHIF iisaidie hospitali hiyo kwa kukopesha vifaa tiba ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi sambamba na watumishi watakaopelekwa hospitalini hapo wenye uwezo mkubwa, hasa kwa kuzingatia kwamba Arusha ni mji wa utalii na huduma zinazotolewa zinapaswa kuwa za viwango vya kikanda.