Customer Feedback Centre

Ministry of Health

COMORO YAAHIDI KULETA WAGONJWA WA SARATANI OCEAN ROAD

Posted on: November 7th, 2025

Na WAF, Dar es Salaam

Rais wa Bunge la Comoro, ambaye pia ni kiongozi wa pili kwa wadhifa katika Serikali ya nchi hiyo, Bw. Moustadroine Abdou, ameahidi kuhakikisha wananchi wote wa Comoro wanaosumbuliwa na maradhi ya saratani wanafikishwa nchini Tanzania kupatiwa matibabu kwenye Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).

Akizungumza wakati wa ziara fupi aliyoifanya Novemba 06, 2025 katika taasisi hiyo, Bw. Abdou amesema amevutiwa na kiwango cha teknolojia ya kisasa inayotumika na hospitali hiyo.

Amesema, kutokana na ubora huo, hakuna tena sababu kwa serikali ya Comoro kutumia fedha nyingi za walipa kodi kuwasafirisha wagonjwa kwenda Ulaya, kwani ORCI ina uwezo wa kutoa tiba bora na kamili.

Aidha, Bw. Abdou amesisitiza umuhimu wa Watanzania kuendeleza amani na utulivu vilivyopo nchini, akibainisha kuwa hali hiyo ndiyo msingi wa maendeleo na utoaji wa huduma bora za afya, jambo linaloweza kuvutia wagonjwa kutoka mataifa mengine ya Afrika na kwingineko.

Kiongozi huyo ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake kubwa za kuimarisha huduma za afya nchini na kuwezesha ORCI kuwa na vifaa vya kisasa, huku akiahidi kuwa Serikali ya Comoro itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuendeleza sekta ya afya na ustawi wa wananchi.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Said Yakubu, amesisitiza kwamba Tanzania ipo tayari kuendeleza ushirikiano na Comoro kwenye nyanja mbalimbali, ikiwemo afya, na akibainisha kuwa hatua hiyo itaimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili rafiki.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dkt. Diwani Msemo, alimshukuru Bw. Abdou kwa kufanya ziara hiyo, akisema kuwa ujio wake ni ishara ya kuimarika kwa ushirikiano baina ya taasisi hiyo na Serikali ya Comoro. Aliongeza kuwa ORCI ipo tayari kushirikiana na Comoro katika kutoa huduma bora kwa wagonjwa wake wote.