Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SAA 120 ZA UTOAJI HUDUMA ZA MATIBABU ZA KIBINGWA MKOANI SHINYANGA,

Posted on: June 17th, 2024Na WAF - SHINYANGA


Kambi ya Madaktari Bingwa wa Mama Samia imewasili mkoani Shinyanga tayari kwa kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, katika Halmashauri zote Sita za Mkoa kuanzia Juni 17 hadi Juni 22.


Hilo limebainika wakati wa uzinduzi wa kambi ya Madaktari Bingwa hao Juni 17,2024, Mkoani Shinyanga zoezi lililofanywa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa huo Frola Kajumla, ambapo amesema timu hiyo ya madaktari bingwa itawafikia hadi wananchi wa pembezoni ili tu kufikisha huduma za kibingwa na kuimarisha Afya zao.


Kajumla pia amemshukuru Rais Samia kwa kufikisha Timu hiyo ya Madaktari Bingwa katika Mkoa huo na kutoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga, wajitokeze kwa wingi kwenye Kambi za Madaktari hao Bingwa, ambao wamesambaa kwenye Halmashauri zote ili wapate matibabu ya kibingwa.


Dkt. Everine Maziku ni Mratibu wa Timu ya Madaktari Bingwa kutoka Idara ya Afya,Uzazi,Mama na Mtoto Wizara ya Afya, amesema Madaktari 30 watawafikia wananchi kwa Huduma ambazo zitakuwa za Magonjwa ya Wanawake, Watoto, Upasuaji,Mkojo,Ganzi, Usingizi, Macho, Mifupa, Mionzi na Magonjwa ya Ndani.


DKT. Maziku ameongeza kuwa tangu Madaktari hao waanze kutoa huduma hizo za kibingwa, tayari wameshafika katika Mikoa 20 na kutoa huduma za Matibabu kwa wananchi zaidi 50000, pamoja na kuwajengea uwezo watoa huduma za Afya wapatao 3,500.


Kwa upande wao wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wamemshukuru Rais Samia, kwa kuendelea kujali wananchi wake kwa kuhakikisha wanaendelea kuwa na Afya Njema, kwamba licha ya kuboresha huduma za Afya nchini, bado ameendelea kuwapelekea na Madaktari Bingwa hadi pembezoni mwa Miji.