MKOA WA SHINYANGA WAPOKEA MADAKTARI BINGWA 47 WA RAIS SAMIA
Posted on: November 4th, 2024
Na WAF - Shinyanga
Mkoa wa Shinyanga leo tarehe 4 Novemba, 2024 umepokea Madaktari Bingwa 47 wa Rais Samia ambao watatoa huduma za matibabu ya kibingwa katika hospitali za halmashauri zote za mkoa huo kwa muda wa siku sita.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya madaktari hao Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Faustine Mulyutu amesema, madaktari bingwa hao watatoa huduma za kibingwa kuanzia tarehe 4 hadi 9 Novemba, 2024.
"Tumepokea madaktari wa upasuaji, mifupa, mfumo wa mkojo, magonjwa ya watoto, magonjwa ya ndani, madaktari wa usingizi, wauguzi wabobezi na madaktari wa meno ambao watatoa huduma kwenye halmashauri zote za mkoa wetu," amesema Dkt. Mulyutu.
Dkt. Mulyutu amesema huduma hizo zinatarajiwa kuwafikia wananchi zaidi ya 4500 katika kipindi ambacho Madaktari hao watakuwa mkoani hapo, hivyo ametoa wito kwa wananchi kufika katika hospitali za halmashauri zao kwa muda uliopangwa ili kupata huduma.
Aidha, Dkt. Mulyutu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na viongozi wa Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kupeleka huduma hiyo kwa awamu ya pili ili wananchi waendelee kupata huduma za kibingwa kwa karibu zaidi.
Naye Mratibu wa zoezi hilo kutoka Wizara ya Afya Bi. Evaline Maziku amesema malengo ya kampeni hiyo ni kuwasogezea wananchi huduma za kibingwa kwenye maeneo yao, kuwajengea uwezo watoa huduma waliopo na kuanzisha huduma za kibingwa ambazo hazijaanza kufanyika mkoani humo.
"Timu ya madaktari imejipanga na sisi Wizara tumejipanga pia tuna imani kuwa wananchi wamejipanga kufika katika vituo vya kutoa huduma, bahati nzuri mkoa wa shinyanga watu wanahamasika sana, kwani hata awamu ya kwanza wagonjwa walijitokeza wakutosha," amesema Bi. Maziku
Kwa niaba ya madaktari bingwa hao Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Dkt. Misana Yango amesema wamejipanga kutoa huduma bora za kibingwa kwa wananchi na pia kuwajengea uwezo watoa huduma katika vituo vyao ili huduma hizo ziwe endelevu vituoni hapo.