Customer Feedback Centre

Ministry of Health

KCMC KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA, KUKABILI MSONGAMANO

Posted on: March 4th, 2025
  1. Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, ameitaka Hospitali ya Rufaa Kanda KCMC kuwekeza zaidi katika upanuzi wa huduma za afya ili kufikia hadhi ya hospitali ya taifa, lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa wananchi wanaosafiri kwenda Dar es Salaam kufuata matibabu ya ngazi ya juu.


Akizungumza wakati wa siku  maadhimisho ya ya Usikivu Duniani yaliyofanyika leo Machi 03, 2025 hospitalini hapo na kuhudumia zaidi ya watu 1,600, Dkt. Mollel amesema, upatikanaji wa huduma bora na  muhimu KCMC utapunguza ongezekoo la watu hospitali kubwa za kitaifa kama Muhimbili, Mloganzila, MOI na JKCI, lakini pia kupunguza gharama na usumbufu wa safari ndefu kwa wananchi na kuokoa fedha zao.


"KCMC, inatakiwa kumaliza rufaa zote ambazo zinapelekwa Dar es Salaam na ili kunusuru uchumi wa watu wetu na wapate muda wa kuhudumiwa ndugu wakiwa karibu," amesema Dkt. Mollel.


Aidha, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na hospitali za rufaa kuboresha miundombinu na kuimarisha upatikanaji wa vifaa tiba ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora bila changamoto za kiusafiri.


Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wataalam wa afya, viongozi wa hospitali na wanajamii waliofika kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya matatizo ya usikivu.