Customer Feedback Centre

Ministry of Health

DHARURA ZAIDI YA 2000 ZAPATA HUDUMA KUPITIA M-MAMA

Posted on: November 1st, 2024

Na, WAF-Dodoma

Dharura 2816 za uzazi kutoka Halmashauri za Mkoa wa Pwani zimefanikishwa kwa kutumia mfumo wa m-mama tangu kuanza kutumika kwa mfumo huo kuanzia Septemba 15, 2023 na kuwezesha kuepusha vifo vinavyotokana na uzazi.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel Novemba 01, 2024 bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe. Subira Khamis ambae alitaka kujua Serikali imejipangaje kuanzisha mpango wa m-mama katika visiwa vya Kibiti, Mafia na Mkuranga ili kupunguza vifo vya mama wajawazito.

“Mkoa wa Pwani ulianza kutumia mfumo wa M-Mama tangu Septemba 15, 2023 ambapo hadi kufikia sasa jumla ya dharura 2816 kutoka katika halmashauri zote za mkoa wa Pwani zimefanikishwa kwa kutumia mfumo wa m-mama ambao umeepusha vifo vinavyotokana na uzazi ,” amesema Dkt. Mollel.

Aidha Dkt. Mollel amesema kupitia mfumo huo Mkoa wa Pwani umeingia mkataba na madereva ngazi ya jamii 112 ikihusisha madereva 14 kutoka halmashauri za Kibiti na Mafia wanaotumia boti ambao wamesafirisha wagonjwa wa dharura katika Halmashauri zote za mkoa huo.

Pia, Dkt. Mollel amesema kuwa mfumo huo unafanya kazi katika maeneo yote ya nchi, hivyo amewaomba waheshimiwa wabunge kuhamasisha wananchi juu ya matumizi ya Namba 115 wawapo na dharura itokanayo na uzazi wakati wa ujauzito, kujifungua na hadi siku 42 baada ya kujifungua na kwa mtoto mchanga siku 0-28.