Customer Feedback Centre

Ministry of Health

BILIONI 1.2 ZAPATIKANA KATIKA HARAMBEE YA HOSPITALI AMANA

Posted on: October 26th, 2024


Jumla ya Shilingi Bilioni 1.2 zimekusanywa katika harambee ya uchangiaji kwa ajili ya upanuzi na ukarabati wa majengo ya mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana.

Hafla hiyo ya uchangiaji iliyofanyika tarehe 25 Oktoba 2024 katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam, imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, ikiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, ambaye alimuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla hiyo.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Simbachawene amesema Hospitali ya Amana imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za afya, hivyo ina haki ya kupokea michango ya kijamii ili kuendeleza juhudi zake.

“Ni wajibu wetu kuichangia hospitali ya Amana si tu kwa ajili ya miundombinu bali pia kwa huduma nyingine zinazohitajika kwa wananchi, lakini ni muhimu zaidi kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa jamii,” amesema Mhe. Simbachawene.

Pia amesisitiza kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya, na kuwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kuunga mkono juhudi hizo.

Awali, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, ameeleza kuwa Rais Dkt. Samia amekuwa kinara katika kuboresha huduma za afya nchini, akionyesha kuwa juhudi zake zimefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama kutoka zaidi ya 500 hadi 104 kwa mwaka, na kuvuka malengo ya Shirika la Afya Duniani (WHO).

“Rais Samia amekuwa mstari wa mbele, na mafanikio haya yameifanya nchi yetu kuvutia wadau wa kimataifa hadi kutamani kukutana naye kwa lengo la kumpa nishani ya heshima kutokana na juhudi zake,” amesema Dkt. Mollel.

Kutokana na michango iliyopatikana katika harambee hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Afya inatarajia kuboresha zaidi huduma katika hospitali hiyo, ikiwemo upanuzi wa majengo ya mama na mtoto, ili kuimarisha huduma kwa wagonjwa na kupunguza msongamano unaoathiri utoaji wa huduma za afya kwa ufanisi.