Customer Feedback Centre

Ministry of Health

ALIYETESEKA NA UVIMBE KWA MIAKA SABA APATA MATIBABU KWA MABINGWA WA SAMIA

Posted on: October 31st, 2024

Na WAF - Njombe

Madaktari Bingwa na Bobezi wa Rais Samia wamefanikiwa kumtoa uvimbe kwenye kizazi mama mwenye umri wa miaka 35 uliomsumbua kwa zaidi ya miaka saba na kumsababishia kushindwa kupata mtoto.

Hayo yamebainishwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya wanawake na uzazi Dkt. Ndaki kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro aliye ongoza jopo la Madaktari kwenye upasuaji huo na kuutoa uvimbe.

Dkt. Ndaki amesema wakiwa katika kampeni ya madaktari bingwa huku wakiweka kambi katika Hospitali za Halmashauri na kuwasogezea wananchi huduma za kibingwa na bobezi walipokea mwananchi aliyekuwa akilalamika kuwa na maumivu kwenye kizazi na baada ya vipimo ilibainika ana uvimbe kwenye kizazi na uvimbe mwingine sehemu ya kuzalisha mayai (ovari).

“Jana wakati tukiendelea na shughuli zetu za kutoa huduma za kibingwa na bingwa bobezi tulipokea mama mwenye umri wa miaka 35 ambaye amekua akiteseka na uvimbe kwenye kizazi kwa muda wa miaka saba hali ambayo ilimsababishia kushindwa kushika ujauzito na kutopata mtoto", amesema Dkt. Ndaki.

Ameongezea kuwa baada ya kukutana na mgonjwa huyo na kujua shida ya uvimbe aliyokuwa nayo waliongea nae na kumshauri kuwa kutokana na uvimbe wake ni kisababishi kinachosababisha kushindwa kupata mtoto.

“Mgonjwa huyu baada ya kumuelezea faida za upasuaji wa kutoa uvimbe huo kwenye kizazi na kukubali tulimpumzisha wodini jana na leo tukamfanyia upasuaji tunashukuru umeenda salama,” amefafanua Dkt. Ndaki.

Akizungumza mara baada ya upasuaji huo mzazi mwenzie Bw. Mbonisye Poka amesema anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujali wananchi wake na kuwasogezea huduma za ubingwa na ubingwa bobezi.

“Mke wangu ameteseka na uvimbe kwenye kizazi kwa mda mrefu na kusababisha tukakosa watoto lakini baada ya kusikia mabingwa wamekuja hatukukata tamaa kuja kuwaona na kuwaelezea shida ya mgonjwa na wakatushauri inabidi kufanyiwa upasuaji na tukakubali tunashukuru mgonjwa amefanyiwa upasuaji na ametoka salama", ameeleza Bw. Mbonisye Poka.