Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YAENDELEA KUIMARISHA UTAYARI WA KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MILIPUKO KAKONKO

Posted on: August 20th, 2026

Na WAF – KIGOMA

Wizara ya Afya, kupitia Kitengo cha Dharura na Maafa kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, imeendelea na ziara ya kukagua na kutathmini maeneo tengefu katika Hospitali ya Wilaya ya Kakonko, Mkoani Kigoma, kwa lengo la kubaini mapungufu na kuyafanyia kazi ili kuimarisha utayari wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko, hususan Ebola.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo leo Agosti 20,2026 Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma Dkt. Erick Richard kutoka Wizara ya Afya, amewataka wahudumu wa Hospitali ya Wilaya ya Kakonko, ambayo ni hospitali teule kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa na wanaoshukiwa kuwa na Ebola, kuhakikisha wanakuwa tayari wakati wote kutoa huduma kwa wananchi

Dkt. Erick amesema Wizara ya Afya itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa magonjwa ya milipuko, ikiwemo Ebola, ili kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kwa wakati endapo kutabainika mgonjwa au mtu anayeshukiwa kuwa na ugonjwa huo.

Dkt.Erick amesema kuwa Mikoa ya Kigoma na Kagera imepewa kipaumbele katika maandalizi ya utayari wa kukabiliana na milipuko kutokana na kuwa karibu na nchi jirani ambazo zimewahi kukumbwa na ugonjwa wa Ebola.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Dharura katika Hospitali ya Wilaya ya Kakonko amesema Wilaya yake imejiandaa vizuri kukabiliana na magonjwa ya milipuko, baada ya mafunzo na uhamasishaji kufanyika kwa makundi mbalimbali, yakiwemo viongozi wa dini, watu mashuhuri pamoja na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.

Ameongeza kuwa, ziara hiyo pia imekuja kuimarisha zaidi maandalizi yaliyokwisha fanyika, sambamba na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho, amesisitiza kuwa Hospitali hiyo itatekeleza maelekezo na ushauri uliotolewa na wataalamu kutoka Wizara ya Afya ili kuendelea kuimarisha utayari na ubora wa huduma zinazotolewa.

Naye Mratibu wa Maambukizi katika Hospitali ya Wilaya ya Kakonko, Swaumu Said, amesema mafunzo na zoezi la maandalizi lililofanyika limewajengea uwezo zaidi wahudumu wa afya katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko,amesema hatua hiyo itawawezesha kuwa tayari kutoa huduma salama na kwa wakati kwa wagonjwa.