Wizara Ya Afya

VIONGOZI WA DINI, MILA WAOMBWA KUFIKISHA TAARIFA ZA KUKABILIANA NA MVUA ZA EL NIÑO NA UGONJWA WA EBOLA ‎ ‎

Posted on: September 24th, 2026

‎Na WAF – SHINYANGA.
‎
‎Viongozi wa dini, wakiwemo Mapadri, Wachungaji na Mashehe wameombwa kutumia nafasi zao kuwaandaa waumini na jamii zinazowazunguka kuchukua tahadhari za kukabiliana na mvua za El Niño na Ugonjwa wa Ebola.
‎
‎Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Peter Masindi Septemba 23, 2026, wakati akizungumza na timu kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI na wadau mbalimbali waliopo mkoani humo kwa ajili ya kufanya , Uhamasishaji na Ushirikishwaji wa jamii wakati wa dharura za mvua za El Niño na Ugonjwa wa Ebola (EVD).
‎
‎Amesema viongozi wa dini na Kimila wana nafasi kubwa ya kufikisha ujumbe wa tahadhari kwa wananchi kutokana na kuwa na mikusanyiko ya waumini na jamii katika maeneo yao.
‎
‎“ tumezungumza na viongozi wa madhehebu wakiwemo Mapadri, Wachungaji na Mashehe kwa ajili ya kuwaambia waumini wao wajue kwamba mwaka huu ni mwaka wa mvua hivyo, maandalizi hayo ni muhimu kwa kuwa mvua kubwa zinaweza kuwalazimisha wananchi kutafuta maeneo salama ya muda ikiwemo shule na nyumba za ibada ,”alisisitiza Mhe. Masindi.
‎
‎Katika hatua nyingine, Mhe. Masindi amesema Wilaya ya Kishapu  imeanza maandalizi ya kukabiliana na changamoto za kiafya zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua kubwa, akieleza kuwa tayari amezungumza na Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) kuhakikisha dawa za kutosha zinakuwepo, hususan kwa ajili ya magonjwa ya mlipuko  ikiwemo Ebola na magonjwa mengine kama hayo yanayoweza kusabaishwa na mafuriko
‎
‎Ameongeza kuwa wataalamu wanaendelea na maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua hizo, huku Wilaya hiyo ikiangalia pia namna ya kutumia rasilimali zilizopo katika shughuli za uokoaji ikiwemo miundombinu, hususan barabara, kama ikitokea itaathirika.
‎
‎Aidha Alisisitiza kuwa gari lililopo katika kitengo cha uokoaji linaweza kutumika kusaidia maeneo yatakayokwama na kuathirika na mvua hizo zinazotarajiwa kunyesha.