Wizara Ya Afya

WATAALAM KILOLO DC MGUU SAWA KUTOA ELIMU KWA WANANCHI JUU YA KUKABILIANA NA EBOLA, EL NIÑO

Posted on: September 25th, 2026

Na Atley Kuni, WAF-Kilolo, Iringa

Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI na Wadau UNICEF na TIP wamefanya zoezi maalum la tathmini ya mfumo wa uratibu wa shughuli za afya kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo shabaha ikiwa ni kuona utayari wa timu hiyo, hususan kwenye kipindi hiki cha tishio la ugonjwa wa Ebola pamoja na uwepo wa mvua za El Nino.

Akiongoza zoezi hilo Septemba 25, 2026 kiongozi wa timu ya Wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Bi. Chipole Mpelembe, amesema shabaha ya zoezi husika ni kuona utayari wa Halmashauri wakati wa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na tishio la magonjwa ya mlipuko na athari za mvua za El Nino.

"Tunafanya zoezi hili kwasababu yakupunguza athari zinazoweza kujitokeza, kwani kinga ni bora kuliko tiba, tukijipanga vizuri wakati huu ambao hali ni shwari, itatusaidia kuepuka athari husika", amesema Bi. Chipole.

Chipole ameongeza kuwa tathmini hiyo, inaeangalia mifumo iliyopo ya uratibu wa shughuli za afya, utayari wa Halmashauri, ushirikiano baina ya wataalamu pamoja na namna taarifa na maelekezo yanavyoratibiwa na kufikishwa kwa wahusika katika kipindi hiki.

Zoezi hilo ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Afya za kuimarisha utayari na mifumo ya uratibu wa afya katika ngazi za Halmashauri, ili kuhakikisha mamlaka husika zinakuwa tayari kuchukua hatua za dharura na kukabiliana na changamoto za kiafya zinazoweza kujitokeza .