Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA , WADAU WAWEKA MIKAKATI YA KUPUNGUZA VIFO VYA WATOTO NCHINI

Posted on: September 24th, 2026

Na Zakayo Mosha WAF-Morogoro

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali imeendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuboresha utoaji wa huduma za Afya kwa watoto na watoto wachanga kwa lengo la kupunguza vifo nchini ifikapo mwaka 2030.

Hayo yamesemwa leo Septemba 24, 2026 mkoani Morogoro na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Christina Guveti wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili cha Wadau na Wataalam wanaojishughulisha na shughuli za mapambano dhidi ya vifo vya watoto na watoto wachanga nchini.

Amesema hadi sasa Serikali kupitia Wizara ya Afya imeweka uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Afya hususani katika ujenzi wa miundombinu mipya ya Hospitali, Vituo vya Afya, Zahanati pamoja na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa.

"Katika Mkoa wetu wa Morogoro Halmashauri zote 8 zinapokea fedha kila mwaka kutoka Serikalini kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na ujenzi wa Vituo vya kutolea huduma za Afya zikiwemo ujenzi wa wodi za watotoa", amesema Dkt. Christina.

Amesisitiza kuwa hali ya utoaji huduma za afya kwa watoto imeimarika kwa sasa kutokana na Serikali kufanya uwekezaji mkubwa Sekta ya Afya kwa kushirikiana na Wadau, amewaomba wadau zaidi kujitokeza kuungana na Serikali katika mapambano ya kupunguza vifo vya watoto na watoto wachanga nchini.

Kwa upande wake Bi. Naomi Chamhene Mratibu wa huduma za afya ya mtoto kutoka Wizara ya Afya amesema wadau na Wataalam hao wanakutana siku mbili Septemba 24-25, 2026 kwa lengo la kupitia utekelezaji wa Afua mbalimbali za Afya ya mtoto, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya kuboresha huduma za Afya ya mtoto.

Amesema kutokana na Takwimu za TDHS za Mwaka 2022 vifo vya watoto wachanga ni 24 katika kila vizazi hai 1000,amesisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imeweka mikakati na mpango wa kupunguza vifo hivyo vifikie vifo 12 katika kila vizazi hai 1000 ifikapo mwaka 2030.