WIZARA YA AFYA YATOA MAFUNZO IGAWILO DC KUIMARISHA UTAYARI WA KUKABILIANA NA EBOLA
Posted on: October 27th, 2026Na Happyness Hans, WAF - Mbeya
Hospitali ya Wilaya ya Igawilo mkoani Mbeya imeimarisha utayari wake wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko, hususan Ebola, kufuatia ziara ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya iliyolenga kutathmini mazingira ya hospitali na uwezo wa watumishi katika kuwahudumia wagonjwa endapo ugonjwa huo utatokea nchini.
Akizungumza leo Oktoba 27, 2026 mkoani Mbeya, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Igawilo, Dkt. Conrad Gazulo, amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa katika kuboresha mazingira ya kutolea huduma na kuwajengea watumishi uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko,amesema Wataalam hao wametoa ushauri na maelekezo kuhusu namna ya kuandaa mazingira salama yatakayomlinda mgonjwa pamoja na mtumishi wa afya wakati wa utoaji wa huduma.
Dkt. Gazulo ameongeza kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kuelewa hatua sahihi za kumhudumia mtu anayeshukiwa kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola, matumizi sahihi ya vifaa vya kujikinga na tahadhari zinazopaswa kuzingatiwa ili kuzuia uwezekano wa maambukizi kuenea.
Aidha, amesema elimu hiyo imewasaidia kutambua mambo muhimu ya kuzingatia na yale ya kuepuka ili kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama na huduma zinazotolewa zinazingatia viwango vinavyotakiwa.
Kwa upande wake, Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Igawilo, Bw. Pascal Haule, amesema ujio wa wataalamu hao umewapa fursa ya kujifunza kwa vitendo na kuongeza uelewa kuhusu maandalizi ya kukabiliana na Ebola.
Amesema wameelekezwa namna sahihi ya kutenga eneo maalumu kwa ajili ya kumuweka mtu anayeshukiwa kuwa na maambukizi, pamoja na hatua za kujikinga na kuzuia kuenea kwa maambukizi ndani ya hospitali.
Bw. Haule ameeleza kuwa mafunzo hayo yamejumuisha pia mbinu sahihi za kunawa mikono, matumizi ya vifaa vya kujikinga na namna ya kuandaa mpango kazi wa muda mfupi utakaosaidia kuimarisha utambuzi wa mapema wa watu wenye viashiria vya ugonjwa huo.
Imeelezwa kuwa Juhudi zinazoendelea kufanyika zinaendana na azma ya Serikali kupitia Wizara ya Afya ya kuimarisha mifumo ya afya, kuongeza uwezo wa watumishi na kuboresha usalama.