Wizara Ya Afya

RAIS SAMIA ANG'ARA UNGA 2026, APONGEZWA KILA KONA KUWA KINARA WA MAMA NA MTOTO

Posted on: September 25th, 2026

Na John Mapepele– New York

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema uwekezaji unaofanywa na Serikali chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan umeiwezesha Tanzania kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto, pia kusogeza huduma za dharura za uzazi na watoto wachanga karibu zaidi na wananchi huku mataifa mbalimbali wakipongeza hatua hiyo.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo Septemba 24, 2026 jijini New York, Marekani wakati akimkaribisha Makamu wa Rais Mhe.Deogratius Njedembi azungumze kwa niaba ya Mhe. Rais Samia katika mkutano uliofanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 81 wa Umoja wa Mataifa (UNGA 2026),

Mgeni rasmi wa mkutano huo Rais wa Namibia Mhe.Netumbo Nandi-Ndaitwah alimpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa aliyoifanya katika eneo la mama na mtoto na kumhakikishia kuwa kwa kazi nzuri inayofanyika Namibia itaendelea kuwa bega kwa bega na Tanzania.

Rais na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Kimataifa linaloshughulika na Afya la Jihpiego Dkt. Allyson Bear katika majadiliano amempongeza Rais Samia kwa mikakati mizuri ya kuokoa maisha ya watoto wachanga na akina mama huku akizitaka nchi nyingine kuiga kwa Tanzania

Aidha, Mhe. Mchengerwa ameeleza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na dhamira ya kisiasa, uwekezaji katika mifumo ya afya pamoja na kuimarishwa kwa huduma zinazolenga kuokoa maisha ya akina mama na watoto.

Amesema juhudi hizo zilianza kupewa msukumo mkubwa mwaka 2018 wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa Makamu wa Rais, alipoanzisha kampeni ya “Jiongeze Tuwavushe Salama” iliyohamasisha viongozi na wadau kuongeza juhudi na rasilimali katika kuhakikisha akina mama wanapata huduma salama wakati wa ujauzito na kujifungua.

“Haikuwa kaulimbiu tu, ilikuwa ni uhamasishaji wa dhamira na rasilimali na ndiyo iliyoweka msingi wa mafanikio tunayoyaona leo, Serikali imeendelea kuwekeza katika watu na mifumo kwa kukarabati vituo vya afya, kutoa mafunzo na kusambaza watumishi wa afya, kuboresha upatikanaji wa dawa pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa utendaji.” amesema Mhe. Mchengerwa