RUFIJI DC YAENDELEA KUCHUKUA TAHADHARI ZA KUKABILIANA NA UGONJWA WA EBOLA,MVUA ZA EL NINO
Posted on: September 25th, 2026Halmshauri ya Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani, imeendelea na zoezi la tathmini ya uwezo wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola na athari za El Nino, kwa lenga kubaini mapema kiwango cha maandalizi na maeneo yanayohitaji maboresho kabla ya dharura kutokea.
Akizungumza leo Septemba 25,2026 Wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani wakati wa zoezi hilo Dkt.Francis Marwa amesisitiza umuhimu wa Wataalam hao kuzingatia mafunzo yaliyotolewa pamoja na kuzingatia tathimin iliyofanyika.
Aidha, ameeleza kuwa tathmini hiyo inafanyika kwa kutumia orodha maalum ya vigezo inayosaidia kuchunguza uwezo wa Halmashauri katika utambuzi wa mapema wa viashiria vya ugonjwa,amesisitiza kuwa utoaji wa taarifa sahihi na kwa wakati kwa jamii utasaidia kuongeza mwitikio wa haraka wakati wa dharura.
"Kwa sekta ya afya sisi tumejipanga na leo tumeendelea na zoezi la kufanya tathimini hapa Rufiji lakini hatukuishia kufanya tathimini tu bali tumetoa na elimu ya namna gani tunaweza kukabiliana na majanga haya mawili ambayo ni El nino na Ugonjwa wa Ebola." amesema Dkt.Francis
Kwa upande wa El Nino, zoezi hilo linaangalia pia namna mifumo ya afya na jamii ilivyojiandaa kukabiliana na changamoto zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa na athari zake kwa huduma za afya, mazingira na maisha ya wananchi.
amesema kuwa zoezi hilo linatekelezwa na Wizara ya Afya kupitia Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu–Sera, Uratibu na Bunge pamoja na UNICEF, Save the Children na TIP.
Dkt.Francis amesisitiza ,matokeo ya tathmini hiyo yanatarajiwa kutoa picha halisi ya hali ya maandalizi ya Rufiji, kubainisha mapengo yaliyopo na kusaidia kuweka vipaumbele vya hatua za maboresho kulingana na mahitaji ya Halmashauri na jamii kwa ujumla.
Amefafanua kuwa, kufanyika kwa tathmini hiyo kabla ya dharura kutokea, Halmashauri ya Rufiji inalenga kuhakikisha kuwa mifumo ya tahadhari, taarifa, elimu na mwitikio inakuwa tayari kutumika kwa wakati, hivyo kupunguza athari zinazoweza kujitokeza wakati wa dharura.