Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WANANCHI DAR ES SALAAM WAHIMIZWA KUJITOKEZA KUCHUNGUZA MABUSHA.

Posted on: January 8th, 2026

Na WAF, Dar es Salaam

Wananchi katika Mkoa wa Dar es Salaam na Mikoa Jirani wamehimizwa kujitokeza kuchunguza Mabusha na kupata huduma bure ya upasuaji wa ugonjwa huo.

Rai hiyo imetolewa leo Januari 8 ,2026 na Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salam Mhe. Albert Chalamila Wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Kambi ya Upasuaji wa Mabusha iliyoanza tarehe 5 hadi 30 Januari, 2026.

"Nitoe rai kwa Wananchi wa Dar es Salaam na mikoa jirani kujitokeza kuchunguza afya zao hasa uchunguzi wa Mabusha na endapo atabainika matibabu yanatolewa bila malipo yanagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100 na lengo ni kufanya upasuaji wa Mabusha kwa zaidi ya Wananchi 500" amesema Mhe. Mtambule

Kwa upande wake Mganga Mkuu mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Mohammed Manuna amesema hadi sasa jumla ya Wananchi 165 wamefanyiwa uchunguzi wa Mabusha huku 127 wakibainika na tatizo hilo na 27 wakiwa tayari wameshafanyiwa huduma ya upasuaji.

"Karibu asilimia moja ya wagonjwa wanapata changamoto ya Mabusha na hadi sasa wananchi 165 wamefanyia uchunguzi huku 127 wakibainika na Mabusha na 27 walishafanyiwa upasuaji ni kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Mikoa jirani ikiwemo Morogoro, Pwani na Lindi.

Naye Meneja Mpango wa Taifa wa Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele Kutoka Wizara ya Afya Dkt.Clara Mwansasu amesema lengo la Serikali ni kuwafikia Wagonjwa 1700 kufanyiwa upasuaji wa Mabusha katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara na Morogoro.