Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA YAIMARISHA MAPAMBANO YA USUGU WA VIMELEA DHIDI YA DAWA

Posted on: February 4th, 2026

Na WAF - Geneva, Uswisi


Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kutekeleza Mpango wa Pili wa Kitaifa wa Kukabiliana na Usugu wa Vimelea Dhidi ya Dawa (NAP AMR 2023–2028), unaoendana na Mpango wa Dunia wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na kusimamiwa kupitia Kamati ya Kitaifa ya Uratibu wa Sekta Mtambuka.


Akizungumza leo, Februari 04, 2026, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, amesema Tanzania pia inaendelea kutekeleza Azimio la Kisiasa la Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2024 kwa kuongeza fedha za ndani katika sekta ya afya, hatua iliyochangia kupungua kwa vifo vinavyohusiana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa (AMR) kwa asilimia 10.


"Jitihada hizi zinaenda sambamba na uimarishaji wa maabara na mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa, kuimarisha udhibiti wa maambukizi katika vituo vya kutolea huduma za afya, kuongeza wigo wa chanjo, kuboresha huduma za maji safi na usafi wa mazingira, pamoja na kuhamasisha uelewa wa jamii kuhusu AMR," amesema Dkt. Magembe 


Aidha, Dkt. Magembe amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya bidhaa za afya zisizo na viwango na bandia ni kipaumbele cha Tanzania, akibainisha kuwa bidhaa hizo huathiri matokeo ya matibabu na kuchochea kasi ya usugu wa vimelea dhidi ya dawa, hali yenye athari kubwa kiafya na kiuchumi.


Pia, Amefafanua kuwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) inaendelea kuimarisha tathmini ya bidhaa kabla ya kuingia sokoni, kufanya ufuatiliaji baada ya matumizi, doria za mara kwa mara, kutumia mifumo ya tahadhari za haraka, pamoja na kutekeleza kampeni za uhamasishaji kwa umma.


Katika kukabiliana na changamoto ya AMR na bidhaa bandia za afya, Tanzania imekijita katika kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya dawa nchini kama njia mojawapo ya kudhibiti bidhaa  bandia. Aidha, Tanzania  imesisitiza umuhimu wa uongozi wa WHO katika usimamizi na ulinganifu wa mifumo ya takwimu ili kuhakikisha ubora wa taarifa, mwingiliano wa mifumo na kufanya maamuzi sahihi yanayolenga kulinda afya ya Watanzania.