Wizara Ya Afya

VIONGOZI WA DINI, WATU MASHUHURI KIGOMA WAAHIDI KUWA MABALOZI WA ELIMU YA TAHADHARI DHIDI YA EBOLA

Posted on: July 21st, 2026

Na Atley Kuni, WAF – Kigoma

Viongozi wa dini na watu mashuhuri mkoani Kigoma wameahidi kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko, ikiwemo Ebola.

Ahadi hiyo imetolewa leo, Julai 21, 2026, na washiriki wa mafunzo ya siku moja yaliyoandaliwa kwa ushirikiano baina ya Serikali na CIHEB Tanzania chini ya mradi wa Usalama wa Afya Duniani na kuwatanisha viongozi wa dini na watu mashuhuri wapatao 35 kutoka Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma.

Wakizungumza wakati wa majadiliano, washiriki hao walikiri kuwa kutokana na ukaribu wa mkoa wa Kigoma na nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kumekuwa na mwingiliano wa watu pamoja na upokeaji wa mizigo kutoka nchi hizo. Hata hivyo, walieleza kuwa kabla ya mafunzo hayo hawakuwa na uelewa wa hatua sahihi za kuchukua ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko.

Katibu wa Chama cha TLP na mfanyabiashara, Jumane Hamis Jumanne, alisema amekuwa akipokea mizigo mbalimbali bila kuzingatia kanuni za usafi wa mikono, jambo ambalo sasa ametambua kuwa linaweza kuongeza hatari ya maambukizi.

“Mimi nimekuwa nikipokea mizigo, mingine midogo na mingine mikubwa, lakini nilikuwa sitilii maanani suala la kunawa mikono kwa maji safi na salama kwa kutumia sabuni baada ya kupokea mizigo hiyo. Badala yake nilikuwa naendelea na shughuli zangu. Kumbe hiyo ilikuwa ni hatari,” amesema Jumanne.

Kwa upande wake, kiongozi wa dini kutoka Msikiti wa Kitongoni, Maneno Rugaba, alisema atatumia elimu aliyoipata kuwafikishia waumini wake ili kuongeza uelewa kuhusu njia za kujikinga na Ebola.

“Nawaomba ndugu zangu mje msikitini kwetu Kitongoni mkazungumze na waumini wenzangu. Mara nyingi husemwa kuwa nabii hakubaliki nyumbani, lakini nina imani mkija mtakuwa chachu ya mabadiliko na watu wataelewa zaidi,” amesema Rugaba.

Naye Beatrice Pascal, mkazi wa Kigoma Ujiji ambaye pia ni mmoja wa watu mashuhuri walioshiriki mafunzo hayo, amesema elimu waliyoipata imewajengea uwezo wa kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu hatari ya ugonjwa wa Ebola na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kujikinga na maambukizi.