Wizara Ya Afya

VIONGOZI WA DINI, WATU MASHUHURI WAHIMIZWA KUREJESHA NA KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA KUNAWIA MIKONO

Posted on: July 22nd, 2026

Na Atley Kuni, WAF – Kigoma DC

Viongozi katika ngazi zote wamehimizwa kurejesha na kuimarisha miundombinu ya kunawia mikono katika maeneo ya kutolea huduma, taasisi za umma, masoko, vituo vya mabasi, nyumba za ibada na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu, kama ilivyofanyika kwa mafanikio wakati wa janga la COVID-19.

Rai hiyo imetolewa leo, Julai 22, 2026, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wakati wa mafunzo yanayo ratibiwa na Waelimishaji kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na mdau wa maendeleo CIHEB Tanzania kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani.

Mafunzo hayo yanalenga kutoa elimu ya kujikinga na kuchukua tahadhari endapo kutatokea mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza, ikiwemo Ebola.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Muelimishaji kutoka Wizara ya Afya, Patrick Makao, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kipindi hiki cha hali ya utayari, kwani unawaji wa mikono kwa maji tiririka na sabuni ni miongoni mwa njia bora za kujikinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa ya mlipuko, yakiwemo Ebola.

"Tunasisitiza pia matumizi ya vibuyu chirizi. Hakikisheni vinahuishwa na kuwekwa katika maeneo muhimu ili wananchi wapate fursa ya kunawa mikono wakati wote," amesema Makao.

Naye Muelimishaji Baraka Mwasandende, amesema kuwa wakati wa janga la COVID-19, vifaa hivyo vilitoa mchango mkubwa wa kuimarisha usafi binafsi na wa mazingira, na vinaendelea kuwa nyenzo muhimu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa mbalimbali.

Aidha, amewataka viongozi kuhakikisha miundombinu hiyo inafanya kazi ipasavyo na wananchi wanaendelea kuhamasishwa kuitumia kwa usahihi, sambamba na kujenga utamaduni wa kunawa mikono.

Kikosi kazi cha utoaji wa elimu kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na mdau CIHEB Tanzania kupitia Mradi wa Usalama wa Chakula Duniani kinaendelea na kampeni ya utoaji elimu katika mikoa ya Kigoma na Kagera huku Viongozi wa dini, watu mashuhuri na wanahabari, watafikiwa ili kuwa mabalozi wa kueneza elimu ya tahadhari dhidi ya Ebola katika maeneo yao ya kazi.