Wizara Ya Afya

WAZIRI MKUU DKT. MWIGULU, AZIDI KUWAITA WAWEKEZAJI SEKTA YA AFYA NCHINI

Posted on: September 9th, 2026

Na Aisha Swahibu, WAF - Arusha

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwingulu Nchemba amesisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya kwa wakati na bila vikwazo vya kifedha.

Dkt. Mwigulu ametoa msisitizo huo wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi (PHC), 2026, unaofanyika leo Septemba 9, 2026 jijini Arusha, unaolenga kujadili namna ya kuimarisha mifumo ya afya na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs),

Amesema kuwa, Tanzania imepiga hatua ya kuongeza upatikanaji wa huduma za afya, kuanzia ngazi ya msingi hadi Taifa.

“Hatua hizi zimeenda sambamba na jitihada za Serikali kuboresha ubora na ufanisi wa huduma pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu karibu na maeneo wanayoishi,” amesema Dkt. Mwigulu

Aidha, amesema Serikali imeendelea kuongeza uwekezaji wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha mfumo wa afya na kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje. Jitihada hizo pia zinalenga kuongeza uwezo wa ndani katika uzalishaji na upatikanaji wa bidhaa muhimu za afya.

Pamoja na mafanikio hayo, Dkt. Mwigulu amesema kuwa bado kuna changamoto kwa baadhi ya viashiria vya afya, hivyo upo umuhimu wa kuendelea kutumia ushahidi wa kisayansi, kushirikiana na wadau wa maendeleo na kuongeza rasilimali katika sekta ya afya, hatua hizo ni muhimu ili kuhakikisha huduma bora na zenye usawa zinawafikia wananchi wote.

“Mkutano huo unatoa fursa kwa Tanzania, Afrika na jumuiya ya kimataifa kutafakari hatua zilizofikiwa na kuweka mikakati ya pamoja ya kuhakikisha malengo ya afya yanafikiwa ifikapo mwaka 2030,” amesema Dkt. Mwigulu

Aidha, Dkt. Mwigulu ameendelea kusisitiza umuhimu wa uwekezaji endelevu katika sekta ya afya kama msingi wa kuboresha ustawi wa wananchi na kufanikisha malengo ya kitaifa, kikanda na kimataifa.