Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TANZANIA NA GLOBAL FUND KUENDELEA KUSHIRIKIANA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI

Posted on: February 6th, 2026

Na WAF - Geneva, Uswisi


Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe amekutana na timu ya Mfuko wa Dunia (Global Fund) iliyoongozwa na Mkurugenzi wa Fedha, Mark Edington, jijini Geneva, ili kujadili namna bora ya kuendelea kuboresha huduma za afya nchini. 


Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Februari 05, 2026 uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 158 wa Bodi Tendaji ya Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Magembe aliishukuru Global Fund kwa ushirikiano wake endelevu na mchango wake mkubwa katika kufadhili programu za Kifua Kikuu, UKIMWI na Malaria, hususan kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wananchi wa Tanzania.


"Sisi kama Serikali tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuhakikisha huduma hizi zinaendelea kuwa endelevu, ikiwemo kuandaa mpango wa haraka wa kuimarisha afua muhimu chini ya programu hizi, hasa katika kipindi hiki cha kupungua kwa misaada ya kimataifa," amesema Dkt. Magembe


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha wa Global Fund, Mark Edington  ameelezea  furaha yake kwa utekelezaji thabiti na mikakati madhubuti ambayo Tanzania imeendelea kutumia katika kuendeleza huduma za UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria bila kuyumba, licha ya changamoto za kifedha.


Aidha, Global Fund ilipongeza juhudi za Tanzania katika kuwekeza rasilimali za ndani ili kulinda mafanikio yaliyopatikana na kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kuwafikia wananchi.


Zaidi ya hayo, Global Fund ilishauri Tanzania kuandaa andiko maalum linaloonyesha mafanikio na uzoefu wake katika utekelezaji wa programu hizi, ili liwe rejea na funzo kwa nchi nyingine duniani.