TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA 158 WA BODI TENDAJI WHO GENEVA
Posted on: February 4th, 2026Na WAF - Geneva
Tanzania imeshiriki katika Mkutano wa 158 wa Bodi Tendaji ya Shirika la Afya Duniani (WHO) unaofanyika Geneva, Uswisi kuanzia tarehe 2 hadi 7 Februari 2026, ukiwa ni maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 79 wa WHO utakaofanyika Mei 2026.
Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, kwa kushirikiana na Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Geneva, Balozi Dkt. Abdallah Saleh Possi, pamoja na wataalamu wa afya kutoka Wizara ya Afya na Ubalozi wa Tanzania Geneva.
Kupitia mkutano huo, Tanzania imewasilisha mikakati mbalimbali ikiwemo kukabiliana na majanga ya kiafya, magonjwa yasiyoambukiza, afya ya akili, utekelezaji wa chanjo, kifua kikuu, magonjwa yasiyopewa kipaumbele, afya kwa wote, afya ya msingi pamoja na mapambano dhidi ya usugu wa vimelea kwa dawa.
Aidha, Tanzania imewasilisha pendekezo la azimio la 'Smart Pharmacovigilance' linalolenga kuimarisha ufuatiliaji wa usalama wa dawa, likizingatia kuwa asilimia kubwa ya vifo vitokanavyo na madhara ya dawa hutokea katika nchi zinazoendelea.
Sambamba na hilo, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe anatarajiwa kukutana na wadau muhimu wakiwemo Global Fund na UNITAID kwa ajili ya kujadili kuimarisha ushirikiano, ufadhili wa programu za Malaria, Kifua Kikuu na UKIMWI pamoja na uzalishaji wa bidhaa za afya ndani ya nchi.