Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI, WADAU WAIMARISHA HUDUMA ZA 'WASH' KUPITIA MFUMO WA AFYA SS

Posted on: February 5th, 2026

Na WAF, Tanga


Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la Center for International Health, Education, and Biosecurity Tanzania (CIHEB-Tanzania), Wameendelea kuimasha huduma za Usafi wa mazingira na usafi binafsi ili kumlinda mwananchi 


Hayo yamebainika wakati wa kikao kazi cha siku tatu cha kuhuisha na kujumuisha zana ya Maji, Usafi wa Mazingira na Usafi wa Kibinafsi (WASH FIT) katika mfumo wa AfyaSS, kwa lengo la kuboresha usimamizi na ufuatiliaji wa huduma za afya nchini.


Kikao kazi hicho, kinachofanyika kuanzia Februari 03 hadi 05, 2026 jijini Tanga katika Ukumbi wa Hoteli ya Mount Usambara, kinatekelezwa kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani. 


Wizara inalenga kuimarisha upatikanaji wa taarifa sahihi na za wakati kuhusu huduma za WASH katika vituo vya kutolea huduma za afya, hatua itakayoongeza ufanisi wa maamuzi na usalama wa huduma kwa jamii.


Kupitia ujumuishaji wa zana ya WASH FIT kwenye mfumo wa AfyaSS, Wizara ya Afya inalenga kuimarisha usimamizi shirikishi na ufuatiliaji endelevu wa viwango vya maji, usafi wa mazingira na usafi wa kibinafsi katika vituo vya afya, hususan kwa jamii zilizo katika mazingira hatarishi.


Hatua hii pia inatekeleza matakwa ya Umoja wa Mataifa (UN) kwa nchi wanachama kutumia zana ya WASH FIT katika kufuatilia na kuhakiki viashiria vya Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDGs), hususan vinavyohusu huduma za maji na usafi wa mazingira katika vituo vya kutolea huduma za afya.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi hicho, Dkt. Chrisogone German kutoka Kitengo cha Uhakiki Ubora wa Huduma za Afya, Wizara ya Afya, amewataka washiriki kushiriki kikamilifu katika mawasilisho na majadiliano ili kuhakikisha matokeo yenye tija na endelevu. Kauli hiyo iliungwa mkono na Dkt. Siril Kullaya, Mkurugenzi wa Ufundi kutoka Mradi wa Usalama wa Afya Duniani – CIHEB Tanzania, aliyesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau katika kuboresha huduma za afya.


Kikao kazi hicho kimewakutanisha washiriki kutoka taasisi kadhaa zikiwemo Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, Mradi wa Usalama wa Afya Duniani – CIHEB Tanzania, pamoja na wataalam kutoka Timu za Usimamizi wa Afya za Mkoa wa Tanga na Halmashauri za Tanga Jiji na Mkinga.