Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DKT. MAGEMBE, MKURUGENZI WHO KANDA YA AFRIKA WAJADILIANA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI

Posted on: February 6th, 2026

Na WAF - Geneva, Uswisi


Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, ameongoza ujumbe wa Tanzania kufanya majadiliano na Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Prof. Mohamed Yakub Janabi, juu ya uboreshaji wa huduma za afya Barani Afrika ikiwemo nchini Tanzania.


Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Februari 05, 2026 pembezoni mwa Mkutano wa Bodi Tendaji wa WHO, ujumbe wa Tanzania ukishirikiana na Balozi wa Kudumu wa Tanzania Geneva, Mhe. Amb. Abdallah Saleh Possi, ulimpongeza Prof. Janabi kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya katika kuimarisha mifumo ya afya barani Afrika.


Ujumbe huo pia uliomba kuimarisha mikakati ambayo Tanzania inaweza kuendelea kuitumia katika kutimiza ajenda ya kuanzisha na kuimarisha uzalishaji wa bidhaa za afya ndani ya nchi (local manufacturing), kwa kuzingatia uzoefu wa nchi nyingine.


Aidha, katika majadiliano hayo, wamejadili namna bora kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) inaweza kupanua wigo wa utekelezaji wa afua za usimamizi wa bidhaa za afya nchini. 


Kufuatia majadiliano hayo, Prof. Janabi na wataalamu wa Tanzania wanaofanya kazi WHO walishauri Wizara ya Afya Tanzania iweze kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Viwanda na Biashara ili kusukuma mbele ajenda ya uzalishaji wa bidhaa za afya ndani ya nchi, pamoja na kuanzisha ubia na nchi zilizoendelea katika eneo hilo kama India, China na Algeria.


"Pia, Tunashauri Tanzania kufanya utafiti wa bidhaa zinazotengenezwa na nchi jirani kama Kenya na Rwanda ili kupanua masoko, kushirikisha sekta binafsi katika mchakato wa uzalishaji, pamoja na kuanzisha kitengo maalum cha 'Resource Mobilization' kwa ajili ya kutafuta rasilimali kutoka kwa wadau," amesema Prof. Janabi


Katika hatua nyingine, Prof. Janabi ameshauri Tanzania kumtumia mtaalamu mshauri aliyewahi kusaidia Ghana kuboresha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote (UHC) kutoka asilimia 28 hadi 60, pamoja na kuruhusu mtaalamu mmoja kutoka Ofisi ya WHO Tanzania kukaa Wizara ya Afya kwa ajili ya kujenga uwezo zaidi.