MUHIMBILI MPYA KUFUTA VIKWAZO VYA HUDUMA ZA TIBA BOBEZI
Posted on: August 20th, 2026Na Shaban Juma, WAF – Dodoma
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mradi wa Ujenzi na Uboreshaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa lengo la kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi nchini.
Dkt. Samizi amesema hayo leo Agosti 20, 2026, wakati akieleza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, akibainisha kuwa ujenzi wa Muhimbili Mpya ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya za kisasa na zenye viwango vya kimataifa.
Amesema mradi huo unalenga kukabiliana na changamoto zinazotokana na ongezeko la wagonjwa wanaohitaji huduma za kibingwa na ubingwa bobezi pamoja na uchakavu wa baadhi ya majengo na miundombinu iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Hospitali ya Taifa Muhimbili imekuwa ikipokea wagonjwa wanaohitaji huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kutoka maeneo mbalimbali nchini na nchi jirani, hali inayoongeza mahitaji ya miundombinu ya kisasa na uwezo wa kutoa huduma kwa wakati.
Dkt. Samizi amesema kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha hospitali hiyo kuongeza na kuanzisha huduma mbalimbali za kibingwa na ubingwa bobezi, zikiwemo upandikizaji figo, tiba radiolojia, upasuaji wa tundu dogo, huduma za wagonjwa mahututi, huduma za dharura, upandikizaji mimba na upandikizaji uloto.
Aidha, amesema mradi huo utasaidia kuimarisha mafunzo ya wataalamu wa afya pamoja na tafiti zinazohitaji teknolojia za kisasa, huku Muhimbili ikilenga kuwa kituo cha umahiri katika huduma za kibingwa na kuchangia kukuza utalii tiba katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.