Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

ZINGATIENI MLO KAMILI KUEPUKA MAGONJWA- RC RUVUMA

Posted on: November 20th, 2025

Na WAF, Ruvuma


Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, amewahimiza wananchi kuzingatia lishe bora ili kuepuka magonjwa yanayotokana na ulaji duni wa lishe.


Hayo yamesemwa leo, Novemba 21, 2025, katika maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa, yaliyofanyika katika Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.


“Mkoa wa Ruvuma umepata heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa. Hizi ni jitihada za Rais wetu, Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha nchi yetu inakuwa na wananchi wenye afya bora,” amesema Brig. Jen. Abbas.


Brig. Jen. Abbas amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuunganisha wadau mbalimbali ili kuendelea kuelimisha na kuhamasisha umma kuhusu lishe bora, pamoja na kueleza athari za utapiamlo katika maendeleo ya taifa kiuchumi na kijamii.


Aidha, amewasisitiza wataalam wa afya kushirikiana kwa pamoja katika kuelimisha umma juu ya umuhimu wa lishe bora pamoja na kuwasihi wananchi kuwa wazalendo na kuipa kipaumbele amani ya nchi.


Kwa upande wake  Mkurugenzi Msaidizi wa Lishe kutoka Wizara ya Afya, Bi. Neema Joshua, amesema lishe ni muhimu kwa afya ya watu wa makundi yote na rika zote. 


Amesisitiza kuwa kila kundi linapaswa kuzingatia lishe bora ili kujenga taifa lenye watu wenye afya bora, jambo litakalosaidia kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.


Maadhimisho hayo yameenda sambamba na kaulimbiu isemayo: “Afya ni mtaji wako: Zingatia unachokula.”