ZAIDI YA MACHO 2,700 YAFANYIWA UPASUAJI WA MTOTO WA JICHO
Posted on: September 19th, 2025
Na WAF - Songwe
Serikali kupitia Wizara ya Afya chini ya Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Helen Keller International (HKI) imetoa huduma za upasuaji wa mtoto wa jicho kwa watu zaidi ya 2,700 kwa lengo la kufikia 3,500 kwa mwaka 2025 katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe na Songwe.
Mwakilishi wa Wizara ya Afya ambaye ni Daktari Bingwa wa Macho Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Johaness Mafwiri amesema hayo leo Septemba 18, 2025 alipotembelea kambi maalumu ya upasuaji wa mtoto wa jicho inayofanyika kwenye Hospitali ya Wilaya Vwawa mkoani Songwe.
"Serikali imekuwa ni mshirika wa wadau na sio mshindani ndio maana tangu kambi hii ianze kwa kushirikiana kwa pamoja tumefikia idadi ya upasuaji wa mtoto wa jicho kwa mwaka huu zaidi ya macho 2,700," amesema Dkt. Mafwiri.
Aidha, Dkt. Mafwiri amesema Mpango wa Taifa wa huduma za macho umekuwa ukitekeleza afua mbalimbali za utolewaji wa huduma za macho nchini kuanzia ngazi ya msingi ambapo hadi sasa imewezesha kurudisha uoni kwa wagonjwa wenye mtoto wa jicho.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Hellen Keller Tanzania Dkt. George Kabona amesema shirika hilo kwa kushirikiana na Serikali lina mpango wa kuwafikia watu 3,500 katika mikoa hiyo ya Iringa, Mbeya, Njombe pamoja na Songwe.
"Tunashirikiana na Wizara ya Afya pamoja na madaktari bigwa wa macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya katika kutekeleza mpango wa kudhibiti ulemavu wa kutokuona unaoepukika hususani unaotokana na ugonjwa wa mtoto wa jicho," amesema Dkt. Kabona.
Amesema, huduma hiyo imekuwa ikitolewa kwa kushirikiana na Serikali ili kutokomeza upofu unaoepukika katika ukanda wa nyanda za juu kusini ili ugonjwa huo uweze kupunguzwa na ikiwezekana kuutokomeza kabisa.
Aidha, ameishukuru Serikali kwa kutoa ushirikiano huo ikiwemo kutoa madaktari bingwa wa macho kwenda kutoa huduma katika kambi hiyo kwa wananchi wenye uhitaji wa kurudishiwa nuru ya kuona na kuendelea na shughuli zao.