WIZARA YA AFYA YAZINDUA UTAFITI WA KITAIFA WA VIASHIRIA VYA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA (STEPS SURVEY 2023)
Posted on: July 20th, 2023Na. WAF Dodoma
Magonjwa Yasiyoambukiza (NCDs) yanachangia takribani 33% ya vifo vyote nchini huku kwa takwimu za Shirika la Afya duniani (WHO) kwa mwaka 2020 zinaonesha kuwa magonjwa hayo yalichangia zaidi ya vifo milioni 41 sawa na 71% ya vifo vyote Duniani ukilinganisha na vifo milioni 57 kwa mwaka 2016 duniani.
Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Afya kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Nassor Mazrui wakati wa Uzinduzi wa Utafiti wa Kitaifa wa Viashiria vya Magonjwa Yasiyoambukiza (STEPS SURVEY 2023) uliofanyika kwenye ukumbi wa Tawimu Jijini Dodoma.
Mhe. Mazrui amesema takwimu zinaonesha kuwa magonjwa hayo yameongezeka mara 5 hadi 9 zaidi kati ya miaka ya 80 ambapo 1% tu ya watanzania walikuwa na tatizo la kisukari na 5% walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu wakati kwa sasa tatizo la kisukari limefikia asilimia 9 na tatizo la shinikizo la juu la damu limeongezeka na kufikia asilimia 25.
“Takwimu hizo zote kutoka katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya nchini zinaonesha ongezeko kubwa sana la magonjwa hayo ambapo katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023, Magonjwa Yasiyoambukiza ambayo yalisababisha wagonjwa wengi kuhudhuria vituo vya huduma za afya ni pamoja na shinikizo la juu la damu wagonjwa 1,456,881 sawa na asilimia 49 ukilinganisha na asilimia 34 kipindi kama hicho mwaka 2021/2022 ,Kisukari wagonjwa 713,057 sawa na asilimia 24, magonjwa ya mfumo wa hewa wagonjwa 386,018 sawa na asilimia 13 ikilinganishwa na asilimia 10 kwa kipindi kama hicho mwaka 2021/2022.
Aidha, amesema katika kukabiliana na ongezeko la magonjwa hayo, Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Afya imeendelea kutekeleza mkakati wa Kitaifa wa kukabiliana na magonjwa hayo nchini kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna bora ya kujikinga na magonjwa hayo pamoja na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma za afya nchini kwa kufikisha huduma za uchunguzi wa awali na matibabu kuanzia ngazi ya afya ya msingi