Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YATINGA NUSU FAINALI SHIMIWI 2026 KWA KISHINDO

Posted on: October 3rd, 2026

Na Zakayo Mosha, WAF – Kilimanjaro

Timu ya mpira wa miguu ya Wizara ya Afya imefuzu hatua ya nusu fainali ya Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Taasisi za Serikali (SHIMIWI) 2026, yanayoendelea mkoani Kilimanjaro, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2–1 dhidi ya timu ya Wizara ya Umwagiliaji.

Akizungumza leo, Oktoba 2, 2026, mkoani Kilimanjaro mara baada ya mchezo huo, Mwenyekiti wa Michezo wa Wizara ya Afya, Bw. Festo Mgata, amesema ushindi huo umetokana na maandalizi mazuri ya timu, nidhamu ya wachezaji na kujituma kwao katika kipindi chote cha mchezo.

Amesema mchezo ulianza kwa timu zote mbili kucheza kwa umakini, huku kila upande ukitafuta nafasi ya kupata bao la kuongoza.

Katika dakika ya 30, mshambuliaji wa Wizara ya Afya, Hamis Bulahya, aliifungia timu yake bao la kwanza kwa shuti kali lililoenda moja kwa moja wavuni.

Bao hilo liliongeza kasi ya mchezo, ambapo katika dakika ya 55, Wizara ya Afya ilipata bao la pili kupitia Hassan Mustapha, aliyefanikiwa kuwazunguka mabeki pamoja na kipa wa Wizara ya Umwagiliaji kabla ya kupeleka mpira wavuni.

Hata hivyo, Wizara ya Umwagiliaji ilipata bao la kufutia machozi katika dakika ya 70 kupitia mkwaju wa penalti.

Licha ya presha kutoka kwa wapinzani wao katika dakika za mwisho, timu ya Wizara ya Afya iliendelea kulinda uongozi wake hadi filimbi ya mwisho ya mwamuzi, na hivyo kuibuka na ushindi wa 2–1.

Akizungumzia hatua inayofuata, Mgata amesema timu hiyo imejiwekea malengo ya kufika fainali na kutwaa Kombe la SHIMIWI 2026.

“Wizara ya Afya mwaka huu tumeandaa timu yetu vizuri na tumejiwekea malengo makubwa ya kufika fainali na kuchukua Kombe la SHIMIWI 2026. Tunaamini tutatimiza malengo hayo chini ya uongozi shupavu wa Waziri wetu wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa,” amesema Mgata.

Amesisitiza kuwa timu hiyo itaendelea kuimarisha maandalizi yake, akieleza kuwa nidhamu, mshikamano na kujituma kwa wachezaji ni miongoni mwa nguzo muhimu zitakazosaidia timu hiyo kufanya vizuri katika hatua zinazofuata.